• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 11:34 AM
Shujaa yajizolea alama 10 Dubai 7s ikimaliza ya nane

Shujaa yajizolea alama 10 Dubai 7s ikimaliza ya nane

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya maarufu kama Shujaa ilimaliza kampeni yake ya Dubai Sevens katika nafasi ya nane hapo jana.

Vijana wa kocha Innocent “Namcos” Simiyu walipigwa 29-7 na Ireland katika mechi ya kuamua nambari saba na nane. Waliambulia alama 10 katika duru hiyo ya kwanza ya Raga za Dunia za msimu wa 2021-2022.Kenya ilianza duru hiyo ya ufunguzi vibaya ilipolimwa na Amerika 14-7 na Argentina 22-17 na kubwaga Uhispania 26-12 katika mechi za makundi.

Ilizabwa 19-5 na Fiji katika robo-fainali na 33-5 mikononi mwa Great Britain katika nusu-fainali ya kuorodheshwa kutoka nafasi ya tano hadi nane. Dhidi ya Ireland, Shujaa ilifungwa miguso kupitia kwa Terry Kennedy (mitatu), Aaron O’Sullivan na Ed Kelly, huku Mark Roche akichangia mikwaju miwili.

Herman Humwa alipachika mguso wa pekee wa Kenya ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Anthony Omondi.Duru ya pili itasakatwa Dubai mnamo Desemba 3-4. Miji mingine itakayoandaa duru saba za mwisho ni Malaga na Seville (Uhispania), Vancouver (Canada), Los Angeles (Amerika), Singapore (Singapore), Toulouse (Ufaransa) na London (Uingereza) mwaka 2022.

Hapo jana, Australia ilimaliza katika nafasi ya tano ilipokung’uta Great Britain 35-21, Ufaransa ikakamata nafasi ya tisa kwa kulima Uhispania 28-26 nayo Japan ikavuta mkia katika nafasi ya 12 baada ya kupepetwa 22-14 na Canada.Mabingwa walitarajiwa kufahamika jana usiku kutoka timu za Argentina, Fiji, Afrika Kusini na Amerika zilizofika nusu-fainali kuu.

You can share this post!

Mwendwa kushtakiwa jumaa tatu

Gunners wakamatia chini Newcastle FC!

T L