• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Siraj apigania kupata namba Harambee Stars

Siraj apigania kupata namba Harambee Stars

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

BEKI wa Bandari FC, Siraj Mohamed amesema atafanya juhudi kuhakikisha anabakia katika kikosi cha timu ya Taifa ya Harambee Stars kitakachovaana na timu za Uganda na Rwanda kwenye kindumbwendumbwe cha mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Siraj ambaye mashabiki wengi walikuwa wanampigia debe achaguliwe kwenye timu ya taifa anasema atafanya bidii kwenye mazoezi ya matayarisho ya mechi hizo ili apate namba katika kikosi cha kwanza.

“Kama walivyo wachezaji wote kuwa na lengo la kuchezea timu ya taifa, nami sina tofauti ndipo nataka nionyeshe wakuu wa benchi la ufundi la Stars kuwa nilistahili kwa kunichagua kwao, hivyo nitafanya bidii na juhudi za mwisho kubakia katika kikosi cha mwisho nipate kucheza,” akasema beki huyo mahiri wa Bandari.

Siraj aliwashukuru wachezaji wenzake, wakuu wa benchi la ufundi na viongozi wa klabu pamoja na mashabiki wa timu yake hiyo ya Bandari na wa jimbo la Pwani kwani anaamini hao ndio waliomfanya afanikiwe kutambulika na kuchaguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa.

“Nawaahidi wote waliochangia kutambulika kwangu kwa maofisa wa Stars kuwa sitawabwaga bali nitafanya bidii za mwisho kuhakikisha ninapata namba ya kucheza na kuonyesha kipaji nilichonacho. Nimekuwa na hamu ya kuvaa jezi ya nchi yangu, nimepata naahidi kuitumikia kwa uwezo wangu wote,” akasema mchezji huyo.

Kuhusu hali ya mchezo wake msimu huu, Siraj amesema haukuwa mbaya ingawa janga la corona lililosababisha kusimamishwa kwa mechi kwa kipindi cha mwezi mmoja unusu kuliathiri kidogo hali ya wachezaji wengi kwa sababu hawakuwa wakifanya mazoezi ya pamoja.

“Nina furaha kuwa baada ya michezo kufunguliwa na kuanza kufanya mazoezi ya pamoja, tumeweza mechi za mwisho kupata matokeo mazuri ambayo yametufanya kumaliza msimu tukiwa nafasi ya tatu. Msimu ujao tutafanya bidii kuhakikisha tunashinda taji la ligi kuu,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Polo 2 wakabana demu akijifungua

Makala ya spoti – Nyika Queens FC ya Taita Taveta