• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Spurs kurefusha mkataba wa Harry Kane ili kuzima ndoto za Man-City na PSG

Spurs kurefusha mkataba wa Harry Kane ili kuzima ndoto za Man-City na PSG

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wameanza mazungumzo na Harry Kane kwa lengo la kushawishi fowadi huyo raia wa Uingereza kutia saini mkataba mpya.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Uingereza alitia saini kandarasi mpya ya miaka sita mnamo 2018.

Hata hivyo, Daniel Levy ambaye ni Mwenyekiti wa Spurs analenga kuchukua tahadhari baada ya vikosi kadhaa maarufu vya bara Ulaya kuanika maazimio ya kujitwalia huduma za Kane mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Manchester City ambao wanaazimia kutafuta kizibo cha fowadi Sergio Aguero ambaye kwa sasa ni mwepesi wa kupata majeraha mabaya, ni miongoni mwa klabu za haiba zinazokeshea maarifa ya Kane.

Kikosi kingine kinachohusishwa na uwezekano wa kumsajili nyota huyo ni Paris Saint-Germain (PSG) baada ya kocha mpya Mauricio Pochettino aliyewahi kumnoa Kane kambini mwa Spurs kudokeza uwezekano wa kuachiliwa kwa chipukizi Kylian Mbappe kuingia kambini mwa Real Madrid nchini Uhispania.

Chini ya kocha Jose Mourinho, Kane mwenye umri wa miaka 27 amekuwa tegmeo kubwa la Spurs huku ushirikiano wake na Son Heung-min ukiwa tishio kubwa kwa mabeki wa timu pinzani katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Carabao Cup na Europa League.

Kane ambaye kwa sasa anadumishwa kwa mshahara wa Sh28 milioni kwa wiki kambini mwa Spurs amefungia waajiri wake mabao 10 na kuchangia mengine 11 ligini msimu huu.

You can share this post!

Hatutaidhinisha ushindi wa Biden, maseneta 11 wasema

Papa Francis akubali kujiuzulu kwa Kadinali John Njue...