• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Hatutaidhinisha ushindi wa  Biden, maseneta 11 wasema

Hatutaidhinisha ushindi wa Biden, maseneta 11 wasema

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

BAADHI ya maseneta nchini Amerika wanasema kwamba watakataa kuidhinisha ushindi wa rais mteule Joe Biden iwapo hakutabuniwa tume ya kuchunguza madai ya wizi wa kura yanayotolewa na Rais Donald Trump.

Maseneta hao 11, baadhi yao waliochaguliwa juzi wakiongozwa na Ted Cruz, wanataka kuidhinishwa kwa matokeo kucheleweshwe kwa siku 10 ili madai ambayo hayana ushahidi yachunguzwe.

Hatua yao haitarajiwi kufaulu kwa sababu idadi kubwa ya maseneta wanatarajiwa kuidhinisha ushindi wa Biden kwenye kikao cha Januari 6.

Trump amekataa kukubali alishindwa na Biden na amekuwa akidai kwamba aliibiwa kura bila kutoa ushahidi wowote. Juhudi zake za kutumia mfumo wa kisheria kubatilisha matokeo zimekataliwa na mahakama. Makamu Rais Mike Pence amekuwa akiepuka kuunga madai ya Trump lakini mnamo Jumamosi mkuu wa wafanyakazi wa ofisi yake Marc Short alisema Bw Pence anaunga juhudi za hivi punde za maseneta kukataa kuidhinisha matokeo Januari 6.

Bunge la Congress inatarajiwa kukutana siku hiyo kuidhinisha matokeo ya kura za majimbo kwenye uchaguzi wa urais wa Novemba 4 mwaka jana.

Matokeo yalionyesha kuwa Biden alimshinda Trump kwa kupata kura 306 dhidi ya 232 za Trump lakini matokeo hayo ni lazima yaidhinishwe na Bunge la Congress shughuli ambayo huwa ni ya kawaida tu.

Baada ya kikao, makamu rais Pence, kwa kutekeleza jukumu lake kama rais wa seneti, atamtangaza Biden kuwa mshindi.

Bw Biden na makamu rais mteule wake, Kamala Harris, wataapishwa Januari 20.

Kwenye taarifa, maseneta 11 wanaoongozwa na Ted Cruz wa Texas walisema kwamba uchaguzi wa Novemba ulikumbwa na madai ya wizi wa kura, ukiukaji wa sheria za uchaguzi na makosa mengine ya upigaji kura. Uchunguzi uliofanywa na idara ya haki (DOJ) haukupata ushahidi wowote kuhusiana na madai ya wizi wa kura.

Wakirejelea hali iliyotokea 1877, ambako kamati iliundwa kufanya uchunguzi baada ya vyama vya Republican na Democratic kudai vilishinda katika majimbo matatu, maseneta hao walihimiza Bunge kuteua tume ya kuchunguza kwa dharura matokeo ya kura na kutoa ripoti yake ndani ya siku 10.

“Uchunguzi ukikamilika, kila jimbo litathmini matokeo ya tume na kuitisha kikao spesheli kuidhinisha mabadiliko yakiwemo,” walisema.

Hata hivyo walisema kwamba wanafahamu ni vigumu juhudi zao kufaulu.

“Tunatarajia wanachama wote wa Democratic na pengine wanachama kadhaa wa Republicans, kukataa,” walisema kwenye taarifa.

Hatua yao ni tofauti na ya seneta wa jimbo la Missouri Josh Hawley, ambaye pia amesema atakataa matokeo ya majimbo akitaja masuala ya uadilifu wa upigaji kura.

You can share this post!

Karua aipinga BBI akiwa katika ngome ya Raila

Spurs kurefusha mkataba wa Harry Kane ili kuzima ndoto za...