• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Spurs wavizia huduma za wakufunzi Hansi Flick na Ralf Rangnick

Spurs wavizia huduma za wakufunzi Hansi Flick na Ralf Rangnick

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wameimarisha juhudi zao za kutafuta kocha mpya kwa kuwaulizia wakufunzi Hansi Flick na Ralf Rangnick kuhusu uwezekano wa kupokezwa mikoba ambayo Jose Mourinho alipokonywa mnamo Aprili 19, 2021.

Spurs kwa sasa wanaongozwa na kocha mshikilizi Ryan Mason aliyewahi kuwa mchezaji wao. Hadi alipokubali kushikilia mikoba ya kikosi cha kwanza, Mason, 29, alikuwa akiwatia makali chipukizi wa akademia ya kikosi hicho.

Chini ya Mason, Spurs wameshinda mechi tatu kati ya nne katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba kwa alama 59 sawa na Everton ambao pia wanafukuzia nafasi ndani ya mduara wa saba-bora ili kufuzu kwa soka ya Europa League msimu ujao.

Kabla ya kuwazungumzia Flick pamoja na Rangnick, Spurs walikuwa wakihusishwa pakubwa na kocha Julian Nagelsmann ambaye atabanduka kambini mwa RB Leipzig ya Ujerumani mwishoni mwa msimu huu na kutwaa mikoba itakayoachwa na Flick kambini mwa Bayern Munich.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian nchini Uingereza, Spurs wamewasiliana na Flick kuulizia iwapo atakuwa radhi kutua jijini London mwishoni mwa msimu huu kudhibiti mikoba yao.

Hata hivyo, mkufunzi huyo ambaye ameongoza Bayern kuhifadhi ufalme wa Bundesliga muhula huu anapigiwa upatu wa kupokezwa mikoba ya timu ya taifa ya Ujerumani baada ya kujiuzulu kwa Joachim Loew mwishoni mwa kampeni za Euro mnamo Julai 11, 2021.

Mbali na Spurs, klabu nyingine inayohemea maarifa ya Flick ni Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, Barcelona watakuwa radhi kumtimua kocha Ronald Koeman mwishoni mwa msimu huu na kumwendea Flick iwapo juhudi zao za kumwajiri kiungo wao wa zamani, Xavier Hernandez, zitagonga mwamba.

Rangnick ambaye ni raia wa Ujerumani, alihusishwa pakubwa na mikoba ya Chelsea kabla ya kikosi hicho kumsajili Thomas Tuchel kuwa kizibo cha Frank Lampard mnamo Januari 2021. Rangnick, 62, aliwahi pia kuwatia makali wanasoka wa Stuttgart, Schalke 04, Hoffenheim na Leipzig.

Wakufunzi wengine wanaohusishwa na mikoba ya Spurs ni Simone Inzaghi wa Lazio, Erik ten Hag wa Ajax, Graham Potter wa Brighton, Brendan Rodgers wa Leicester City na Roberto Martinez wa timu ya taifa ya Ubelgiji.

“Usimamizi utachukua muda kabla ya kuanza mchakato wa kutafuta kocha mpya. Isitoshe, bado hatujaanza shughuli ya kutathmini kuhusu mkufunzi anayefaa zaidi kati ya wengi wanaohusishwa na Spurs kwa sasa,” akasema mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy huku akimsifia kocha Mason ambaye anasaidiwa kazi na Chris Powell, Nigel Gibbs, Ledley King na kocha wa makipa, Michel Vorm.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Walinzi wa rais wamnyaka mwanamume akinyemelea jukwaani Lamu

Kiini cha Uhuru kuteleza nyumbani