• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Tottenham wampa Nuno Espirito Santo mikoba yao ya ukocha

Tottenham wampa Nuno Espirito Santo mikoba yao ya ukocha

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wamemwajiri kocha wa zamani wa Wolves, Nuno Espirito, kwa mkataba wa miaka miwili.

Nuno aliagana na Wolves mnamo Mei 2021 baada ya kuhudumu uwanjani Molineux kwa misimu minne ambapo aliongoza kikosi hicho kutwaa taji la Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) na kutinga robo-fainali za Europa League.

Spurs walimtimua kocha Jose Mourinho mnamo Aprili 19 na kumteua aliyekuwa mkufunzi wao wa kikosi chipukizi, Ryan Mason, 29 kuwa mshikilizi wa mikoba ambayo Mourinho alipokonywa.

“Ni tija na fahari tele kupokezwa mikoba ya Spurs. Nina furaha kubwa wakati huu ninapotazamia kuanza kazi,” akaongeza Nuno.

“Hatuna siku nyingi zaidi za kupoteza. Inalazimu tuanze kazi mara moja kwa ajili ya kujiweka sawa kwa muhula ujao utakaoanza chini ya wiki chache zijazo,” akaongeza kocha huyo raia wa Ureno.

Nuno hata hivyo, hatasubiri sana kabla ya kuongoza Spurs kukutana na waajiri wake wa zamani. Spurs wamepangiwa kumenyana na Wolves uwanjani Molineux mnamo Agosti 22. Huo utakuwa mchuano wao wa pili katika msimu mpya wa 2021-22.

Ambacho hakijabainika kufikia sasa ni iwapo nahodha na fowadi tegemeo, Harry Kane, atasalia kuwa sehemu ya kikosi chake.

Mnamo Mei 2021, Kane ambaye kwa sasa anaongoza timu ya taifa ya Uingereza kwenye kampeni za Euro, aliwataka Spurs kumwachilia kutafuta hifadhi mpya kwingineko. Tukio hilo liliwachochea Manchester City, Manchester United na Real Madrid kuanza kuhemea maarifa yake.

Spurs wamemwajiri Nuno baada ya juhudi zao za kujinasia huduma za Mauricio Pochettino, Antonio Conte, Paulo Fonseca na Gennaro Gattuso kuzaa nunge.

Katika msimu wake wa kwanza uwanjani Molineux, Nuno aliongoza Wolves kutwaa ubingwa wa Championship mnamo 2017-18 kabla ya kuongoza kikosi hicho kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya saba kwa mihula miwili mtawalia. Wolves walikamata nafasi ya 13 kwenye jedwali la EPL mnamo 2020-21.

Nuno anaungana sasa na Fabio Paratici aliyeteuliwa kuwa mkurugenzi wa soka kambini mwa Spurs mwanzoni mwa Juni 2021 baada ya kuagana na Juventus ya Italia.

Siku muhimu katika safari ya Spurs kutafuta kocha mpya:

Aprili 19 – Jose Mourinho afutwa kazi na Spurs baada ya miezi 17

Aprili 20 – Kiungo wa zamani wa Spurs, Ryan Mason, 29, aanza kushikilia mikoba ya ukocha.

Aprili 27 – Julian Nagelsmann wa RB Leipzig aliyepigiwa upatu kuwa kocha wa Spurs aajiriwa na Bayern Munich.

Aprili 30 – Kocha Erik ten Hag aliyehusishwa na Spurs atia saini mkataba mpya na waajiri wake Ajax.

Mei 23 – Kocha Brendan Rodgers wa Leicester City aanza kuhusishwa na Spurs ila anatangaza mpango wa kutojiengua ugani King Power.

Mei 27 – Spurs wamzungumzia kocha Mauricio Pochettino kuhusu uwezekano wake kuondoka PSG na kurejea kambini mwao.

Mei 28 – PSG watangaza kuwa hawana mpango wa kumwachilia Pochettino.

Juni 2 – Kocha Antonio Conte apigiwa upatu wa kuajiriwa na Spurs baada ya kujiuzulu kambini mwa Inter Milan.

Juni 4 – Conte aliyewahi kuwa kocha wa Chelsea akatiza mazungumzo yake na Spurs baada ya kutoafikiana kuhusu udhibiti wa fedha na mpango wa kusajili wachezaji wapya.

Juni 15 – Spurs waanza kumnyemelea kocha wa zamani wa AS Roma, Paulo Fonseca.

Juni 17 – Spurs wakatiza mazungumzo na Fonseca na kuanza kuwasiliana na Gennaro Gattuso aliyevunja ndoa na Fiorentina baada ya siku 23 pekee.

Juni 18 – Mpango wa kuajiriwa kwa Gattuso watibuka baada ya mashabiki kuandamana kupinga mikakati hiyo ya Spurs.

Juni 30 – Mchakato wa kutafuta kocha mpya watamatika na Nuno Espirito Santo aajiriwa na Spurs.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mtoto wako hatarini kutekwa

Moto wateketeza afisi ya naibu kamishna Lari, nyumba za...