• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Tumepiga hatua ya maana, asema kocha wa Shujaa

Tumepiga hatua ya maana, asema kocha wa Shujaa

Na GEOFFREY ANENE

Kocha wa timu ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume, Innocent’Namcos’ Simiyu ameeleza kufurahishwa na hatua ambazo Shujaa imepiga katika maandalizi ya Olimpiki.

Alizungumza na Taifa Leo kutoka nchini Uhispania mnamo Jumatatu kabla ya kufunga safari ya kurejea nyumbani, Namcos alisema vijana wake walicheza vizuri duru mbili za Madrid Sevens.

“Timu ilicheza vizuri. Kwa sasa tunafurahia mahali ambapo vijana wamefika kuhusu safari yetu ya Olimpiki za Tokyo. Tunajua kuna idara tunazofaa kuimarisha kama jinsi ya kuanzisha mpira na ulinzi, lakini nimefurahishwa na idara nyingine kama mashambulizi,” alisema Namcos ambaye enzi zake kama mchezaji aliwahi kuchezea timu hiyo na pia kuwa nahodha.

“Tunarejea Nairobi leo (Jumatatu) na kuanza matayarisho yetu ya duru ya Dubai juma lijalo. Tutaelekea mjini Dubai mnamo Machi 26,” aliongeza.

Nchini Uhispania, Shujaa ilikamata nafasi ya pili katika duru ya kwanza ya Madrid Sevens nyuma ya Argentina mnamo Februari 20-21 na pia kumaliza katika nafasi hiyo katika duru ya pili mnamo Februari 27-28. Mbali na Shujaa na Argentina, kitengo cha wanaume pia kilikuwa na Amerika, Ureno, Uhispania na Chile.

Lionesses, ambayo ni timu ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande ya kinadada, pia ilishiriki duru hizo mbili. Ilikamilisha katika nafasi ya mwisho katika wikendi ya kwanza kabla ya kupoteza dhidi ya Urusi katika fainali ya duru ya pili mnamo Februari 28.

Vipusa wa kocha Felix Oloo,ambao walikutana na Ufaransa, Uhispania, Amerika na Poland, wanatarajiwa kurejea nyumbani na Shujaa leo Jumatatu.

Shujaa na Lionesses zilifuzu kushiriki Olimpiki baada ya Kenya kushinda Kombe la Bara Afrika la wanaume na kumaliza ya pili kwenye dimba la wanawake mwaka 2019.

  • Tags

You can share this post!

Kaizer Chiefs yapepetwa 4-0 na Wydad Athletic

Bitok ataja 20 Malkia Strikers ikijiandaa kuingia kambi ya...