• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Bitok ataja 20 Malkia Strikers ikijiandaa kuingia kambi ya Olimpiki

Bitok ataja 20 Malkia Strikers ikijiandaa kuingia kambi ya Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

Wachezaji wanane kutoka klabu ya KCB wamejumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya voliboli ya wanawake (Malkia Strikers) itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki mwezi Julai/Agosti nchini Japan.

Wanabenki hao ni nahodha Mercy Moim pamoja na Edith Wisa, Sharon Chepchumba, Jemima Siangu, Violet Makuto, Leonida Kasaya, nahodha wa klabu ya KCB Noel Murambi, na Emmaculate Misoki.

Mabingwa wa taifa, Kenya Prisons, wana wachezaji sita kikosini ambao ni Joy Lusenaka, Immaculate Chemtai, Elizabeth Wanyama, Joan Chelagat, Lorine Chebet na Pamela Kepkirui. Agrippina Kundu, Esther Mutinda na Pamela Adhiambo kutoka Kenya Pipeline pia wako katika kikosi cha Malkia Strikers cha wachezaji 20 kitakachoingia kambini katika ukumbi wa Kasarani.

Mwezi Januari 2020, Malkia Strikers ilifaulu kurejea kwenye Olimpiki tangu 2004. Haikufuzu mwaka 2008, 2012 na 2016. Ilishiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza kabisa 2000.

Mabingwa hao mara tisa wa Afrika wanatamani kutwaa ubingwa wa Olimpiki na wameratibiwa kuingia kambini mnamo Machi 11, miezi mitano kabla ya michezo hiyo ya kifahari kuanza jijini Tokyo.

Kocha wa KCB, Japheth Munala, alieleza kufurahi kwake timu yake kuchangia wachezaji wengi katika timu ya taifa na kusema kuwa watasaidia Malkia Strikers kuleta kombe nyumbani.

“Sina tashwishi kuhusu uwezo wao na ninatumai watasaidia timu ya taifa kushinda taji,” alisema Munala.

Murambi alisema anatumai Olimpiki itakuwa ya kufana.

Malkia Strikers, ambayo inanolewa na kocha Paul Bitok, itakuwa kambini kuwa siku 15 kabla ya wachezaji kujiunga na klabu zao kwa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika. Watarudi kambini Aprili halafu waelekee Japan kwa kambi nyingine ya mazoezi ya majuma matatu ambako watacheza michuano kadhaa ya kujipima nguvu kabla ya Olimpiki.

  • Tags

You can share this post!

Tumepiga hatua ya maana, asema kocha wa Shujaa

Chanjo ya corona kutua Nairobi Jumanne