• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Ubelgiji kutegemea masogora tisa wa EPL kwenye fainali za Euro 2021

Ubelgiji kutegemea masogora tisa wa EPL kwenye fainali za Euro 2021

Na MASHIRIKA

JUMLA ya wanasoka tisa wanaotandaza Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 26 kitakachotegemewa na timu ya taifa ya Ubelgiji kwenye fainali za Euro mwaka huu 2021.

Kiungo matata wa Manchester City, Kevin de Bruyne ametiwa katika kikosi hicho kwa pamoja na masogora watatu wa Leicester City – Timothy Castagne, Dennis Praet na Youri Tielemans.

Kikosi hicho cha kocha Roberto Martinez kitajivunia pia maarifa ya fowadi mahiri wa Inter Milan, Romelu Lukaku, na kiungo mzoefu wa Real Madrid, Eden Hazard.

Straika Romelu Lukaku. Picha/ AFP

Ubelgiji kwa sasa wanashikilia nafasi ya kwanza kwenye orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Wametiwa katika Kundi B kwa pamoja na Urusi, Denmark na Finland kwenye fainali za Euro zitakazofanyika kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021.

Wanasoka wengine wanaochezea vikosi mbalimbali vya EPL ambavyo wameitwa kambini mwa Ubelgiji ni beki Toby Alderweireld wa Tottenham Hotspur, fowadi Leandro Trossard wa Brighton, mshambuliaji Christian Benteke wa Crystal Palace na Michy Batshuayi aliyehudumu kwa mkopo kambini mwa Palace kwa mkopo msimu huu kutoka Chelsea.

Licha ya kufanyiwa upasuaji wa misuli ya miguu mnamo Januari 2021, kiungo matata wa Borussia Dortmund, Axel Witsel, pia amejumuishwa katika kikosi cha Ubelgiji.

“Baada ya Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) kutoa idhini kwa washiriki wa Euro 2021 kupanga vikosi vya wanasoka 26 badala ya 23, niliamua kumjumuisha Witsel kwa sababu ni mchezaji aliye na upekee na uwezo mkubwa uwanjani,” akasema Martinez.

Kiungo wa zamani wa Everton na Manchester United, Marouane Fellaini, hajapata fursa ya kuunga kikosi cha Ubelgiji ambacho hakijawahi kumwajibisha tangu ayoyomee China baada ya fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi.

Washiriki wote wa Euro 2021 wana hadi Juni 1, 2021 kuwasilisha orodha ya mwisho ya wachezaji watakaowawakilisha kwenye mashindano hayo.

KIKOSI CHA UBELGIJI:

MAKIPA: Thibaut Courtois (Real Madrid), Simon Mignolet (Club Bruges), Matz Sels (Racing Strasbourg).

MABEKI: Toby Alderweireld (Tottenham Hotspur), Dedryck Boyata (Hertha Berlin), Timothy Castagne (Leicester City), Jason Denayer (Olympique Lyonnais), Thomas Meunier (Borussia Dortmund), Thomas Vermaelen (Vissel Kobe), Jan Vertonghen (Benfica).

VIUNGO: Nacer Chadli (Istanbul Basaksehir), Kevin de Bruyne (Manchester City), Leander Dendoncker (Wolverhampton Wanderers), Thorgan Hazard (Borussia Dortmund), Dennis Praet, Youri Tielemans (wote wa Leicester City), Hans Vanaken (Club Bruges), Axel Witsel (Borussia Dortmund).

WAVAMIZI: Michy Batshuayi, Christian Benteke (both Crystal Palace), Yannick Carrasco (Atletico Madrid), Jeremy Doku (Stade Rennes), Eden Hazard (Real Madrid), Romelu Lukaku (Inter Milan), Dries Mertens (Napoli), Leandro Trossard (Brighton & Hove Albion).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ashtakiwa kufanya kitendo cha kipumbavu ndani ya feri

RIZIKI: Kilimo cha miwa katika eneo la mimea inayochukua...