• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ufaransa wabandua Uingereza na kufuzu kwa nusu-fainali itakayowakutanisha na Morocco

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ufaransa wabandua Uingereza na kufuzu kwa nusu-fainali itakayowakutanisha na Morocco

Na MASHIRIKA

UINGEREZA waliaga Kombe la Dunia mwaka huu katika hatua ya robo-fainali baada ya Ufaransa kuwapepeta 2-1 ugani Al Bayt mnamo Jumamosi.

Nahodha Harry Kane alipoteza penalti muhimu ambayo ingefanya mambo kuwa 2-2 mwishoni mwa kipindi cha pili. Awali, nyota huyo wa Tottenham Hotspur alikuwa amepachika wavuni mkwaju wa penalti na kufikia rekodi ya nguli Wayne Rooney ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Uingereza kwa mabao 53.

Ufaransa waliwekwa kifua mbele na Aurelien Tchouameni aliyevurumisha kombora kutoka hatua ya mita 23 na kumwacha hoi kipa Jordan Pickford.

Uingereza walitamalaki asilimia kubwa ya mchezo na kupata nafasi nyingi za kufunga. Walianza kipindi cha pili kwa matao ya juu na wakapata penalti katika dakika ya 54 baada ya Tchouameni kumwangusha Bukayo Saka ndani ya kijisanduku.

Hata hivyo, Ufaransa walirejea uongozini katika dakika ya 78 baada ya Olivier Giroud kujaza kimiani krosi safi kutoka kwa Antoine Griezmann. Kane alipaisha penalti ambayo ingefanya mambo kuwa 2-2 baada ya Theo Hernandez kumkabili Mason Mount visivyo katika dakika ya 86.

Tukio hilo lilimnyima Kane fursa ya kuvunja rekodi ya Rooney na kuzima ndoto ya Uingereza waliokuwa wakilenga kunyanyua Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1966. Ufaransa ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, sasa watamenyana na Morocco kwenye nusu-fainali mnamo Disemba 14, 2022 ugani Al Bayt.

Mnamo 2018, Uingereza waliaga Kombe la Dunia nchini Urusi katika hatua ya nusu-fainali baada ya kupokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Croatia. Ubelgiji waliwapepeta 2-0 katika pambano la kutafuta mshindi nambari tatu na nne.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mashabiki wa soka jijini Kisumu wapata utamu wa Kombe la...

PAUKWA: Ama kweli nzi kufa kidondani si haramu

T L