• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Uhispania yatema idadi kubwa ya wanasoka wazoefu kikosini

Uhispania yatema idadi kubwa ya wanasoka wazoefu kikosini

Na MASHIRIKA

KOCHA wa timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania, Jorge Vilda, ametema wanasoka nyota katika kikosi kitakachoshiriki michuano miwili ijayo ya kimataifa dhidi ya Uswidi na Amerika.

Nahodha Irene Paredes na mfungaji bora wa muda wote, Jenni Hermoso, ni miongoni mwa wachezaji wazoefu ambao wameachwa nje ya kikosi hicho.

Ni wachezaji tisa pekee kati ya 23 waliowajibishwa kwenye michuano ya Septemba 2022 ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia wamedumishwa kambini.

Wiki moja iliyopita, Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) lilidai kuwa wanasoka 15 waliapa kujiuzulu na kustaafu soka ya kimataifa iwapo Vilda asingepigwa kalamu.

Wanasoka wa Uhispania walikana baadaye kushinikiza RFEF kumtimua Vilda huku shirikisho hilo lilisisitiza kuwa hakuna mchezaji ambaye angeteuliwa kuchezea timu ya taifa kabla ya kuomba msamaha kwa utovu wa nidhamu.

Hermoso amesema hiki ndicho kipindi “kisichopendeza zaidi ambacho kimewahi kushuhudiwa katika historia ya soka ya wanawake nchini Uhispania.”

Wanasoka wa Barcelona Paredes, Patri Guijarro, Mapi Leon, Sandra Panos na Aitana Bonmati, wote wametemwa nje pamoja na mshindi wa taji la Ballon d’Or, Alexia Putellas, anayeuguza jeraha.

Ona Batlle na Lucia Garcia wa wa Manchester United pamoja na Leila Ouahabi na Laia Aleixandri wa Manchester City pia hawakuitwa kambini.

Real Madrid ndicho kinajivunia idadi kubwa ya wanasoka kambini mwa Uhispania. Hakuna yeyote kati ya wanasoka tisa wa Real walioshiriki wala kuhusika katika maandano ya timu ya taifa dhidi ya kocha Vilda.

Uhispania wamepangwa kuchuana na Uswidi mnamo Oktoba 7, 2022 kabla ya kuelekea Amerika siku nne baadaye. Mechi hizo za kupimana nguvu ni sehemu ya maandalizi ya Uhispania kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Australia na New Zealand kuanzia Julai 2023.

Chini ya kocha Vilda, Uhispania walipigwa na Uingereza kwenye robo-fainali za Euro 2022 japo wataanza kupigiwa upatu kuwa malkia wa dunia mwakani iwapo watajumuisha kikosini idadi kubwa ya wanasoka wao wazoefu ambao sasa wametemwa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kilio cha wakazi wa Kariminu vyanzo vya maji safi...

WANTO WARUI: Waziri Machogu endapo ataidhinishwa asitarajie...

T L