• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Uingereza waponda Ukraine na kujikatia tiketi ya kuvaana na Denmark kwenye nusu-fainali za Euro

Uingereza waponda Ukraine na kujikatia tiketi ya kuvaana na Denmark kwenye nusu-fainali za Euro

Na MASHIRIKA

UINGEREZA walionyesha mchezo wa hali juu katika ushindi wa 4-0 waliosajili dhidi Ukraine kwenye robo-fainali ya Euro mnamo Jumamosi usiku jijini Roma, Italia.

Ufanisi huo wa masogora wa kocha Gareth Southgate uliwakatia tiketi ya kumenyana na Denmark kwenye nusu-fainali itakayochezewa uwanjani Wembley mnamo Julai 7, 2021. Denmark walifuzu kwa nusu-fainali baada ya kucharaza Jamhuri ya Czech 2-1 jijini Baku, Azerbaijan.

Three Lions wa Uingereza walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowawezesha kubandua Ujerumani kwa kichapo cha 2-0 kwenye hatua ya 16-bora.

Nahodha Harry Kane aliyefunga mojawapo ya magoli dhidi ya Ujerumani, aliwafungulia Uingereza ukurasa wa mabao dhidi ya Ukraine baada ya kushirikiana vilivyo na Raheem Sterling katika dakika ya nne.

Ukraine walisalia butu katika dakika 30 za kwanza huku Uingereza waliotinga nusu-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi wakipania kufuzu kwa hatua hiyo kwenye mapambano ya haiba kubwa kwa mara ya pili mfululizo.

Sawa na walivyofanya katika kipindi cha kwanza, Uingereza walianza kipindi cha pili kwa matao ya juu na wakafunga mabao mawili ya haraka kunako dakika za 46 na 50 kupitia Harry Maguire na Kane. Mabao hayo yalichangiwa na Luke Shaw ambaye ni beki stadi wa Manchester United.

Bao la nne la Uingereza lilijazwa kimiani na nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson aliyeletwa uwanjani katika kipindi cha pili kujaza nafasi ya Jadon Sancho ambaye sasa ni mali ya Man-United baada ya kusajiliwa kwa Sh12 bilioni kutoka Borussia Dortmund. Goli hilo la Henderson lilichangiwa na chipukizi Mason Mount wa Chelsea.

Mchuano huo ulikuwa wa tano mfululizo kwa Uingereza kusakata kwenye Euro mwaka huu bila ya kufungwa goli.

Masogora wa Southgate walifungua kampeni za Euro kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Croatia kabla ya kuambulia sare tasa dhidi ya Scotland katika mechi ya pili ya Kundi D. Ushindi wa 1-0 waliosajili dhidi ya Jamhuri ya Czech katika mechi ya mwisho kundini uliwapa fursa ya kukutana na Ujerumani kwenye hatua ya muondoano.

Ushindi dhidi ya Denmark utawakatia Uingereza tiketi ya kufuzu kwa fainali ya kipute cha haiba kubwa zaidi kwa mara ya kwanza tangu 1966 walipotawazwa wafalme wa Kombe la Dunia.

Mbali na Kane, mwanasoka mwingine anayejivunia ufufuo mkubwa wa makali yake katika timu ya taifa ya Uingereza ni Shaw aliyesajiliwa na Man-United kutoka Southampton mnamo Juni 2014. Awali, nafasi anayoichezea sasa katika timu ya taifa ilikuwa ikimilikiwa na Ben Chilwell wa Chelsea na Kieran Trippier wa Atletico Madrid.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Tuonane kwenye debe la urais 2022 – Muturi

Messi aongoza Argentina kucharaza Ecuador na kuingia...