• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uruguay waaga mashindano licha ya kukung’uta Ghana 2-0 katika Kundi H

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uruguay waaga mashindano licha ya kukung’uta Ghana 2-0 katika Kundi H

Na MASHIRIKA

JAPO Uruguay walitandika Ghana 2-0 katika pambano lao la mwisho la Kundi H kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Qatar, mabingwa hao mara mbili wa dunia (1930, 1950), waliaga kipute cha mwaka huu katika hatua ya makundi.

Waliambulia nafasi ya tatu kundini kwa alama nne sawa na Korea Kusini waliowapiku kwa wingi wa mabao. Huku Korea Kusini wakijaza kimiani mabao manne kutokana na mechi tatu za Kundi H, Uruguay walifunga mawili pekee.

Ureno walitamalaki kundi hilo ya Korea Kusini kuwalima 2-1 katika mechi ya mwisho.

Kigogo Luis Suarez alichangia mabao yote mawili ambayo Uruguay walifungiwa na Giorgio de Arrascaeta. Hata hivyo, aliondoka ugani akitiririkwa na machozi ikizingatiwa kwamba fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar ndizo zake za mwisho kunogesha katika taaluma yake ya usogora.

Mwishoni mwa mechi, wachezaji wa Uruguay walimchemkia refa kwa madai kuwa aliwanyima penalti baada ya fowadi Darwin Nunez kuangushwa na Alidu Seidu ndani ya kijisanduku.

Ghana walipoteza penalti kupitia kwa mshambuliaji na nahodha Andre Ayew baada ya mkwaju wake kupanguliwa na kipa Sergio Rochet matokeo yakiwa bado 0-0. Penalti hiyo ilitokana na tukio la Mohammed Kudus kuchezewa visivyo na Rochet ndani ya kijisanduku.

Ghana walishuka dimbani wakipania kulipiza kisasi dhidi ya Uruguay waliowabandua kwa hila kwenye robo-fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mnamo 2010.

Wakati huo, Ghana walidenguliwa na Uruguay kwa penalti 4-2 baada ya kuambulia sare ya 1-1 chini ya dakika 120. Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia matuta fowadi Asamoah Gyan alipopoteza penalti mwishoni mwa muda wa ziada baada ya Suarez kunawa mpira ndani ya kijisanduku na kuonyeshwa kadi nyekundu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kutukana polisi wa kike wawili

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Cameroon wafunganya virago Qatar...

T L