• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Vihiga Queens na Gaspo Women kidedea KWPL, Zetech na Bunyore watoshana nguvu

Vihiga Queens na Gaspo Women kidedea KWPL, Zetech na Bunyore watoshana nguvu

NA AREGE RUTH

VIHIGA Queens waliendelea kuganda kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL), baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya WADADIA Women ugani Mumias Sports Complex Kaunti ya Kakamega leo Jumamosi.

Bao la kiungo Maureen Ater katika dakika ya 10,  lilikuwa la manufaa kwa Vihiga ambao sasa wamepanua mwanya kwenye msimamo wa ligi.

Kufikia raundi ya saba, Ater alikuwa mfungaji bora na mabao matano. Hata hivyo, kutokana na kutofunga katika mechi mbili za awali ambazo Vihiga ilipoteza mtawalia, kiungo Wendy Achieng wa Thika Queens ndiye ameshikilia usukani na magoli tisa. Ater amefunga tatu bora na mabao sita.

Baada ya raundi ya tisa, Vihiga wana pointi 19 kutokana na mechi tisa za ligi. Wameshinda mechi sita, wakapiga sare moja na kupoteza mechi mbili. WADADIA nao, wamesalia nafasi ya saba na alama 13.

Ugani Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi, mambo yalizidi unga kwa wanajeshi wa Ulinzi Starlets baada ya kulala mikononi mwa Gaspo Women ambao waliwanyeshea 2-0. Mabao hayo yalifungwa na Emily Andayi na Elizabeth Wamboi.

Meneja wa Gaspo Vivian Akinyi alisema kuwa, “Baada ya kupoteza mechi yetu ya awali, tulirejea nyumbani kurekebisha makosa yetu maeneo ya mashambulizi na mabeki. Ilikuwa ni mechi ngumu kwetu, Ulinzi ni mingoni mwa timu ngumu kwenye ligi kufikia sasa.”

Gaspo wamepanda hadi nafasi ya pili kwenye jedwali na alama 18.

Kwa upande mwingine, Zetech sparks walitoshana nguvu ya 2-2 dhidi ya  Bunyore starlets ugani GEMS Cambridge kaunti ya Kajiado.

Sare hiyo iliwapelekea Bunyore kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye jedwali na alama 16, alama tatu nyuma ya vinara wa ligi Vihiga. Zetech nao wanaendelea kujikokota katika nafasi ya nane na alama 10.

Kiungo Puren Alukwe na Mercy Njeri walifungia Zetech bao kila mmoja,  nao Maria Ambila na Lucy Andacho wakafungia Bunyore. Alukwe anashikilia nafasi ya nne kwenye orodha ya wafungaji bora na magoli sita.

Bunyore, Kangemi Ladies na Kayole Starlets ni miongoni mwa timu ambazo ziliponea kushuka daraja msimu jana. Lakini msimu huu, Bunyore imedhihirisha kuwa na uwezo wa kuendelea kusalia kwenye ligi baada ya kuhangaisha timu kubwa ligini.

Kocha wa timu hiyo Zacharia Zilasi, hakufurahishwa na matokeo hayo.

“Nilitaka sana tupate alama tatu lakini hata alama moja ugenini ni muhimu kwetu. Tulilegea katika kipindi cha pili na tukaadhibiwa na wapinzani wetu, tunarejea nyumbani kurekebisha makosa yetu,” alisema Zilasa.

  • Tags

You can share this post!

Wito magavana waweke sheria kupambana na Kolera

Chelsea watoshana nguvu na West Ham United katika EPL...

T L