• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Chelsea watoshana nguvu na West Ham United katika EPL ugenini

Chelsea watoshana nguvu na West Ham United katika EPL ugenini

Na MASHIRIKA

WEST Ham United waliendeleza masaibu ya Chelsea katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kuwalazimishia sare ya 1-1 uwanjani London Stadium.

Chelsea walitangulia kuona lango la wenyeji wao kupitia kwa Joao Felix katika dakika ya 16 kabla ya West Ham kusawazishiwa na Emerson Palmieri aliyefunga dhidi ya waajiri wake wa zamani dakika 12 baadaye.

Tofauti na West Ham waliolenga kushinda mechi mbili mfululizo za nyumbani kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 2022, Chelsea walipania kukomesha rekodi duni ya kutoshinda mechi yoyote kati ya nane mfululizo ugenini na kupunguzia kocha Graham Potter presha ya kutimuliwa ugani Stamford Bridge.

Baada ya kufunga mwaka wa 2022 kwa kupoteza michuano sita kati ya saba katika mashindano yote, West Ham sasa wameshinda mechi tatu na kupiga sare tatu kutokana na mapambano saba yaliyopita mwaka huu.

West Ham sasa wana alama 20 kutokana na michuano 22 na pengo la pointi 11 linatamalaki kati yao na Chelsea wanaokamata nafasi ya tisa jedwalini. Tangu katikati ya Oktoba 2022, Chelsea wameshinda mechi mbili pekee kutokana na 13 ligini na matumaini yao ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao yanazidi kudidimia.

Isitoshe, wamefunga mabao manane pekee kutokana na mechi 13 zilizopita za EPL na wanajivunia magoli 23 kutokana na mechi 22 za hadi kufikia sasa msimu huu ligini. Ushindi dhidi ya West Ham jana ungalikuwa wao wa tatu mfululizo dhidi ya kikosi hicho kwa mara ya kwanza tangu Aprili 2011.

Chelsea tayari wameaga vipute vya Kombe la FA na Carabao Cup na watarejelea kampeni zao za UEFA mnamo Jumatano dhidi ya Borussia Dortmund katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ugenini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Vihiga Queens na Gaspo Women kidedea KWPL, Zetech na...

Raila angali bado chaguo langu, Uhuru aambia wakazi

T L