• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Vikosi 14 vya EPL vilivyotinga raundi ya nne FA

Vikosi 14 vya EPL vilivyotinga raundi ya nne FA

Na CHRIS ADUNGO

VIKOSI vyote vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) isipokuwa Crystal Palace, Aston Villa, Newcastle United, West Bromwich Albion na Leeds United vilibanduliwa na limbukeni wa soka ya Uingereza kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA msimu huu wa 2020-21.

Palace ndio waliokuwa wa kwanza kuaga shindano hilo kongwe zaidi katika historia ya kandanda ya Uingereza baada ya kung’atwa 1-0 na Wolves mnamo Januari 8 ugani Molineux. Villa nao walibanduliwa siku hiyo baada ya kupepetwa 4-1 na Liverpool uwanjani Villa Park.

Goli la pekee na la ushindi kwa Wolves lilifumwa wavuni na kiungo raia wa Uhispania, Adama Traore. Kwa upande wao, Liverpool walifungiwa na Sadio Mane (mawili), Georginio Wijnaldum na Mohamed Salah huku Villa wakifutiwa machozi na chipukizi Louie Barry, 17.

Mnamo Januari 9, jumla ya mechi 20 zilisakatwa huku ile iliyokuwa iwakutanishe Southampton na Shrewsbury Town uwanjani St Mary’s kuahirishwa baada ya visa vingi vya maambukizi ya Covid-19 kuripotiwa kambini mwa Shrewsbury inayoshiriki Ligi ya Daraja la Pili nchini Uingereza.

Kati ya mechi zilizosakatwa, Arsenal ambao ni mabingwa watetezi na wafalme mara 14 wa Kombe la FA walilazimika kusubiri hadi muda wa ziada kuwapokeza Newcastle kichapo cha 2-0 uwanjani Emirates baada ya pande zote kuambulia sare tasa mwishoni mwa muda wa kawaida wa dakika 90.

Mabao ya Arsenal wanaotiwa makali na kocha Mikel Arteta yalifumwa wavuni na wanasoka Emile Smith Rowe na Pierre-Emerick Aubameyang.

Scott McTominay alifungia Manchester United bao la pekee na la ushindi dhidi ya Watford ugani Old Trafford huku mabao kutoka kwa James Justin, Marc Albrighton, Ayoze Perez na Harvey Barnes yakisaidia Leicester City kuwaponda Stoke City 4-0 uwanjani bet365. Chini ya kocha Brendan Rodgers, Leicester alitandaza mchuano huo bila ya kujivunia huduma za fowadi Jamie Vardy na kiungo James Maddison.

Fulham waliwapiga Queens Park Rangers (QPR) 2-0 ugenini nao Sheffield United wakampunguzia kocha wao Chris Wilder presha ya kupigwa kalamu kwa kuwacharaza Bristol Rovers 3-2. Burnley waliwadengua Milton Keynes Dons kwa mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti baada vikosi hivyo kuambulia sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa ziada uwanjani Turf Moor.

Mambo hayakuwaendea vyema wanasoka wa West Bromwich Albion ambao chini ya mkufunzi Sam Allardyce, walizidiwa ujanja na Blackpool kwa mabao 3-2 kupitia penalti baada ya kuambulia sare ya 2-2 mwishoni mwa dakika 90 za kawaida na 30 nyinginezo za ziada.

Cenk Tosun na Abdoulaye Doucoure walifunga bao kila mmoja na kusaidia Everton ya kocha Carlo Ancelotti kupokeza Rotherham United kichapo cha 2-1 uwanjani Goodison Park.

Jumapili ya Januari 10 ilikuwa zamu ya Chelsea, Manchester City, Tottenham Hotspur, Brighton na Leeds United.

Kocha Frank Lampard aliowaongoza masogora wake wa Chelsea kuwapepeta Morecambe 4-0 kupitia mabao ya Mason Mount, Timo Werner, Callum Hudson-Odoi na Kai Havertz uwanjani Stamford Bridge.

Kwa upande wao, Spurs walizamisha chombo cha Marine kirahisi baada ya Alves Morais almaarufu Carlos Vinicius kufunga mabao matatu katika ushindi wa 5-0. Mabao mengine ya Spurs wanaotiwa makali na kocha Jose Mourinho yalifumwa wavuni na Lucas Moura na chipukizi Alfie Devine, 16.

Chini ya mkufunzi Pep Guardiola, Man-City walizima matumaini ya kusonga mbele kwa Birmingham City baada ya kusajili ushindi wa 3-0 kupitia mabao ya Bernardo Silva (mawili) na Phil Foden.

Kati ya vikosi vya EPL vilivyoduwazwa zaidi katika michuano yote ya raundi ya tatu ya Kombe la FA ni Leeds ambao chini ya kocha Marcelo Bielsa, walipokezwa kichapo kikali cha 3-0 kutoka kwa Crawley Town.

Crawley wanaojivunia huduma za beki raia wa Uingereza mwenye asili ya Kenya, David Sesay, 22, walifungiwa mabao yao na Nick Tsaroulla, Ashley Nadesan na Jordan Tunnicliffe.

Brighton waliwabandua Newport County kwa kichapo cha 4-3 kupitia penalti baada ya vikosi hivyo kuambulia sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa ziada.

You can share this post!

Wiper kumtia adabu Muthama kupitia mke waliyeachana

Wenyeji watawala mbio za Great Ethiopian Run, Wakenya...