• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Vikosi vya raga ya Kenya Cup vyakumbatia mfumo wa mechi za mkondo mmoja kwa ajili ya msimu mpya wa 2020-21

Vikosi vya raga ya Kenya Cup vyakumbatia mfumo wa mechi za mkondo mmoja kwa ajili ya msimu mpya wa 2020-21

Na CHRIS ADUNGO

LIGI Kuu ya Raga (Kenya Cup) ambayo imepangiwa kuanza Februari 13, 2021 itakumbatia mfumo tofauti utakaoshuhudia washiriki wakipiga mechi za mkondo mmoja pekee.

Kwa mujibu wa mpangilio huo mpya, kampeni za Ligi Kuu zitashuhudia jumla ya mechi 11 pekee zikitandazwa kati ya Februari na Mei kabla ya nusu-fainali na fainali kutandazwa katika kipindi cha wikendi mbili zitakazofuata.

Maamuzi hayo ni zao la maafikiano kati ya kamati ya Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) ya kuratibu mechi pamoja na vinara wa vikosi vya Kenya Cup na Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship).

Iwapo kampeni za Kenya Cup kwa minajili ya msimu wa 2020-21 zitaanza Februari, ina maana kwamba klabu zitaanza maandalizi kwa kupiga kambi za mazoezi mnamo Januari mwaka ujao chini ya uzingativu wa kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Kuanza kwa Kenya Cup kutawapa pia wakufunzi wa timu za taifa za Shujaa na Simbas fursa za kuandaa vikosi vyao kwa mapambano yajayo ya Olimpiki na Kombe la Afrika mtawalia.

“Hatua hiyo itapiga jeki maandalizi ya timu za taifa kwa minajili ya mapambano yajayo ya kimataifa,” akasema Xavier Makuba ambaye ni mwenyekiti wa vikosi vya Kenya Cup.

Vikosi vya Kenya Cup havijawahi kushiriki mapambano yoyote tangu Machi ambapo kampeni zote za raga zilisitishwa kwa sababu ya janga la corona.

Wakati huo, Kabras RFC walikuwa kileleni mwa jedwali la Kenya Cup kwa alama 74, tatu zaidi kuliko wanabenki wa KCB ambao ni mabingwa watetezi. Homeboyz, Impala, Mwamba na Menengai Oilers walifuata.

Nafasi za Western Bulls na Kisumu RFC walioshushwa mwishoni mwa msimu wa 2019-20, zitatwaliwa na ama na Strathmore Leos, Mean Machine, USIU, Egerton Wasps au Northern Suburbs katika muhula mpya wa 2020-21.

You can share this post!

Wachangiaji mitandao waliofunga pingu za maisha wachangamka...

Vijana wamzuia Gideon kupokea baraka