• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Wanaraga wa Kenya Simbas wang’atwa na Boland ligi ya Currie Cup

Wanaraga wa Kenya Simbas wang’atwa na Boland ligi ya Currie Cup

NA GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya Simbas imefungwa miguso mitatu katika dakika 15 za mwisho na kupoteza 45-33 dhidi ya wenyeji Boland Cavaliers kwenye ligi ya daraja ya kwanza ya Currie Cup nchini Afrika Kusini, Jumamosi.

Timu hizo zilikuwa 26-26 wakati mechi hiyo ilisimamishwa kwa dakika 15 mchezaji wa Boland akipokea matibabu.

Baada ya mechi kurejea, safu ya ulinzi ya vijana wa kocha Paul Odera ilizidiwa maarifa na kufungwa miguso mitatu ya haraka kabla ya kujiliwaza na mguso wa mwisho kutoka kwa Thomas Okeyo.

Mechi hiyo ilianza kwa Andrew Matoka kuweka Kenya kifua mbele 7-0 kupitia mguso na mkwaju dakika ya tatu.

Boland ilisawazisha 7-7 dakika ya nane ilipopata mguso na mkwaju baada ya Simbas kusalia wachezaji 14 mmoja wao alipolishwa kadi ya njano na kukaa nje.

Timu ya Boland ilichukua uongozi 14-7 kabla ya Vincent Onyala kupunguza mwanya huo hadi 14-12 kupitia mguso dakika ya 25. Mguso wa Eugene Sifuna ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Matoka ulipatia Simbas uongozi 19-14 dakika ya 30.

Samuel Asati alionyeshwa kadi ya njano nje ya kisanduku cha mguso na Boland ikatumia skramu yake vyema kupachika mguso kufanya mambo kuwa 19-19 dakika ya 36. Kipindi hicho kilitamatika 19-19 kabla ya Boland kuanza dakika 40 za mwisho kwa kutinga mguso dakika ya kwanza ya kipindi cha pili ulioandamana na mkwaju kuwa juu 26-19.

Simbas ilisawazisha 26-26 kupitia kwa mkwaju wa Beldad Ogeta ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Geoffrey Ominde. Mechi ilisimamishwa dakika ya 65 kwa dakika 15 ili mchezaji wa Boland apokee matibabu.

Kipindi hicho kinaonekana kilifanya Simbas kupoteza umakinifu kwani mchezo ulipoendelea ilifungwa miguso mitatu kabla ya Simbas kupata mguso wa kujituliza kutoka kwa Okeyo dakika ya mwisho.

Mechi hiyo ilikuwa ya sita ya Simbas ambayo ilipoteza dhidi ya Valke 51-14 Aprili 9, Zimbabwe Goshawks 22-21 Aprili 22, Griffons 66-33 Aprili 30 na kuchapa Border Bulldogs 35-12 Aprili Mei 7. Simbas itavaana na SWD Eagles katika mechi yake ijayo mnamo Mei 28.

  • Tags

You can share this post!

Dortmund wamtimua kocha Marco Rose baada ya msimu mmoja

Serikali yaruhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje

T L