• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Warembo wa Uswidi na Uholanzi waingia robo-fainali za Euro 2022

Warembo wa Uswidi na Uholanzi waingia robo-fainali za Euro 2022

Na MASHIRIKA

MABANATI wa Uswidi walitinga robo-fainali za Euro 2022 mnamo Jumapili kwa kufunga mabao matatu katika kipindi cha kwanza na kusajili ushindi mnono wa 5-0 uliozima matumaini ya Ureno kwenye kipute hicho.

Uswidi wanaoshikilia nafasi ya pili duniani, watarejea ugani Leigh Sports Village, Uingereza, mnamo Ijumaa kuvaana na Iceland, Ubelgiji au Italia katika hatua ya nane-bora.

Mabingwa watetezi, Uholanzi, walikomoa Uswisi 4-1 uwanjani Bramall Lane katika pambano jingine la Kundi C na kujikatia tiketi ya kuvaana na Ufaransa kwenye robo-fainali nyingine mnamo Jumamosi ugani New York Rotherham. Uholanzi walinyanyua taji la Euro kwa mara ya kwanza miaka mitano iliyopita.

Chini ya kocha Petr Gerhardsson, Uswidi walipata mabao yao kupitia kwa Carole Costa aliyejifunga, Kosovare Asllani, Stina Blackstenius na Filippa Angeldal aliyemtatiza sana kipa Patricia Morais aliyekuwa akiwajibishwa na Ureno kwa mara ya kwanza katika kivumbi cha Euro.

Uswidi walishuka dimbani dhidi ya Ureno wakiwa nyuma ya mabingwa watetezi Uholanzi waliofungua nao kampeni za Kundi C kwa sare ya 1-1 mnamo Julai 9. Ingawa Uholanzi walitandika Uswisi, ushindi mnono wa Uswidi dhidi ya Ureno uliwakweza kileleni mwa kundi kwa alama saba, japo kwa wingi wa mabao.

Ureno wanaokamata nafasi ya chini zaidi kwenye orodha ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), waliaga makala ya Euro mwaka huu baada ya kujizolea alama moja pekee kutokana na mechi tatu, sawa na Uswisi.

“Tulitaka kudhihirishia mashabiki ukubwa wa uwezo wetu. Wapinzani sasa wana sababu ya kuhofia kukutana nasi. Tuna motisha tele na lengo letu ni kutwaa taji. Tulicheza vizuri, tukatamalaki mechi na kuwazidi ujanja washindani wetu katika kila idara,” akasema kocha Gerhardsson.

Uswidi wanajivunia ufufuo mkubwa wa makali yao tangu waambulie nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2019 na kuzoa nishani ya fedha kwenye Olimpiki za Tokyo 2020. Walicharaza Ureno siku tatu baada ya kupepeta Uswisi 2-1 katika Kundi C. Hata hivyo, hawakuwa na kiungo mzoefu Caroline Seger aliyekosa mechi ya Euro kwa mara ya kwanza tangu 2005.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa supu ya asparagus

Kepsa yaisihi serikali itengeneze mazingira ya...

T L