• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Watford waajiri kocha Claudio Ranieri kujaza pengo la Xisco Munoz

Watford waajiri kocha Claudio Ranieri kujaza pengo la Xisco Munoz

Na MASHIRIKA

WATFORD wamemteua kocha mzoefu raia wa Italia, Claudio Ranieri, kuwa mrithi wa Xisco Munoz aliyetimuliwa uwanjani Vicarage Road mnamo Oktoba 3, 2021 baada ya kuhudumu kambini mwa kikosi hicho kwa kipindi cha miezi 10 pekee.

Chini ya Munoz ambaye ni raia wa Uhispania, Watford walirejea katika EPL mwishoni mwa msimu wa 2020-21 baada ya kutamalaki kampeni za Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Hadi kutimuliwa kwake, Munoz alikuwa ameongoza Watford kujizolea alama saba kutokana na mechi saba za EPL msimu huu. Matokeo hayo yalikuwa yamewaweka Watford katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa jedwali.

Familia ya Pozzo ambayo inamiliki Watford, inabadilisha kocha wa kikosi hicho kwa mara ya 14 tangu 2012.

Kuajiriwa kwa Ranieri aliyeagana na Sampdoria ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mwishoni mwa msimu wa 2020-21, kutamshuhudia akirejea EPL baada ya kuongoza Leicester kunyanyua ufalme wa kipute hicho mnamo 2015-16.

Kibarua chake cha kwanza akidhibiti mikoba ya Watford ni mechi ya EPL itakayowakutanisha na Liverpool uwanjani Vicarage Road mnamo Oktoba 16, 2021.

Ranieri anajivunia tajriba pevu na uzoefu mpana katika ulingo wa ukufunzi na Watford itakuwa klabu yake ya 21 kusimamia katika kipindi cha miaka 35 iliyopita ya ukocha. Katika kipindi hicho, amenyanyua mataji manane, likiwemo Kombe la Italian Cup alilolitwaa mnamo 1998-1998 akiwanoa Fiorentina pamoja na ufalme wa Super Cup alioutia kapuni mnamo 2004-05 akidhibiti mikoba ya Valencia.

Ranieri ambaye ameajiriwa kwa mkataba wa miaka miwili na Watford, amewahi pia kuwa kocha wa Chelsea na Fulham.

Ingawa anastahiwa pakubwa kambini mwa Leicester, kikosi hicho kilimfuta kazi mnamo 2017 baada ya msururu wa matokeo duni yaliyosaza klabu hiyo na alama moja pekee juu ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho zikisalia mechi 13 pekee kwa msimu wa 2016-17 kutamatika.

Baada ya kutimuliwa na Leicester, alitua kambini mwa Nantes katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kabla ya kurejea EPL kudhibiti mikoba ya Fulham mnamo 2018. Hata hivyo, alihudumu kambini mwa Fulham kwa siku 106 pekee kabla ya kikosi hicho kumpiga kalamu kikiwa katika hatari ya kushuka ngazi kwenye EPL.

Munoz aliyefurushwa na Watford baada ya kikosi chake kupigwa 1-0 na Leeds United mnamo Oktoba 2, 2021, ndiye kocha wa kwanza wa EPL kupigwa kalamu msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Niliwaomba PSG waniachilie ili niyoyomee Real Madrid...

PATA USHAURI WA DKT FLO: Kwa nini mjamzito huvuja damu...