• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Watford waduwaza Everton na kuvunia kocha Ranieri ushindi wa kwanza tangu arejee EPL

Watford waduwaza Everton na kuvunia kocha Ranieri ushindi wa kwanza tangu arejee EPL

Na MASHIRIKA

MABAO matatu kutoka kwa mshambuliaji Joshua King yalisaidia Watford kupepeta Everton 5-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi uwanjani Goodison Park.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Watford kusajili chini ya kocha mpya Claudio Ranieri aliyeaminiwa kuwa mrithi wa mkufunzi Xisco Munoz mwanzoni mwa Oktoba 2021.

Tom Davies aliwaweka Everton kifua mbele katika dakika ya tatu kabla ya King kusawazisha mambo dakika 10 baadaye. Ingawa Richarlson Andrade alirejesha Everton ya kocha Rafael Benitez uongozoni katika dakika ya 63, juhudi zake zilifutwa na Juraj Kucka kunako dakika ya 78.

King ambaye hakufungia Everton bao lolote alipokuwa akichezea kikosi hicho kwa nusu ya kwanza ya muhula uliopita wa 2020-21, alipachika wavuni mabao mawili kwa upande wa Watford katika dakika za 80 na 86 kabla ya Emmanuel Dennis kuzamisha kabisa chombo cha Everton mwishoni mwa kipindi cha pili.

Everton walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kushinda ikizingatiwa kwamba Watford hawakuwa wamewahi kuwapiga katika mchuano wowote uwanjani Goodison Park. Kwa upande wake, ilikuwa mara ya tano mfululizo kwa Ranieri kuongoza kikosi chake kubwaga Everton katika uga wao wa nyumbani.

Kichapo hicho kilikuwa cha pili mfululizo kwa Benitez aliyezomewa vikali na mashabiki kutokana na maamuzi yake ya kuondoa uwanjani fowadi Anthony Gordon na kumleta Richarlson kujaza pengo lake katika kipindi cha pili.

Hata hivyo, Benitez alionekana kujiondoa lawamani Richarlson alipofunga bao dakika tatu pekee baada ya kuletwa uwanjani. Ulegevu wa Everton mwishoni mwa kipindi cha pili uliwezesha Watford kuwafunga mabao manne chini ya dakika 12 za mwisho wa mchezo huo.

Watford walioanza maisha chini ya Ranieri kwa kichapo cha 5-0 kutoka kwa Liverpool mnamo Oktoba 16, 2021, sasa wanashikilia nafasi ya 14 jedwalini kwa alama 10 sawa na Aston Villa. Everton kwa upande wao wanakamata nafasi ya nane kwa alama 14 sawa na West Ham United, Everton na Arsenal.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Man-City yakung’uta Brighton na kupaa hadi nafasi ya...

TSC kupandisha zaidi ya walimu 2,400 vyeo

T L