• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Man-City yakung’uta Brighton na kupaa hadi nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL

Man-City yakung’uta Brighton na kupaa hadi nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

PHIL Foden alipachika wavuni mabao mawili katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ulioshuhudia waajiri wake Manchester City wakichabanga Brighton 4-1 ugani Amex mnamo Jumamosi usiku.

Ushindi huo wa Man-City ambao ni mabingwa watetezi wa EPL uliwapaisha hadi nafasi ya pili jedwalini kwa alama 20, mbili nyuma ya viongozi Chelsea.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walifunga mabao matatu chini ya dakika 30 za kipindi cha kwanza na kuzamisha chombo cha Brighton ambao vinginevyo wangewaruka iwapo wangesajili ushindi.

Man-City waliwekwa kifua mbele na Ilkay Gundogan katika dakika ya 13 kabla ya Foden kucheka na nyavu za wenyeji wao katika dakika ya 28 na 30 mtawalia. Ingawa Alexis Mac Allister alipania kurejesha Brighton mchezoni kupitia penalti ya dakika ya 81, Man-City walipata bao la nne kupitia penalti iliyochanjwa na Riyad Mahrez mwishoni mwa kipindi cha pili.

Foden kwa sasa amepachika wavuni mabao manne akivalia jezi za Man-City muhula huu. Mnamo 2020-21, Brighton walitoka chini kwa mabao mawili na kupepeta Man-City katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL.

Man-City walioanza kampeni za EPL msimu huu kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur, sasa wamefunga mabao 11 na kuruhusua nyavu zao kutikiswa mara mbili kutokana na mechi tatu zilizopita. Wamejizolea jumla ya alama 20 kutokana na mechi nane zilizopita.

Brighton walishuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo wakiwa wamefungwa mabao mawili pekee (bila kuhesabu penalti) baada ya mwanzo bora zaidi katika kampeni za EPL muhula huu. Sasa wanafunga mduara wa tano-bora kwa pointi 15 sawa na Spurs.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Chama pekee si kigezo cha kiongozi bora – Jungle

Watford waduwaza Everton na kuvunia kocha Ranieri ushindi...

T L