• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
West Brom wakaba koo Man-United na kudidimiza matumaini yao ya kutwaa taji la EPL msimu huu

West Brom wakaba koo Man-United na kudidimiza matumaini yao ya kutwaa taji la EPL msimu huu

Na MASHIRIKA

BAO la Bruno Fernandes mwishoni mwa kipindi cha kwanza liliwawezesha Manchester United kujizolea alama moja dhidi ya West Bromwich Albion katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani The Hawthorns.

Hata hivyo, sare hiyo ya 1-1 iliwanyima masogora wa kocha Ole Gunnar Solskjaer fursa ya kufukuzana na viongozi wa jedwali Manchester City huku matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa EPL msimu huu yakididimia hata zaidi.

Kufikia sasa, Man-United wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 46, saba zaidi nyuma ya Man-City ambao chini ya kocha Pep Guardiola, wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimetandazwa na washindani wao wakuu wakiwemo Man-United, Leicester City na mabingwa watetezi Liverpool wanaofunga mduara wa nne-bora kwa pointi 40.

West Brom wanaotiwa makali na kocha Sam Allardyce walijiweka uongozini baada ya sekunde 83 pekee za kipindi cha kwanza kupitia goli la Mbaye Diagne. Bao hilo lilitokana na krosi ya Conor Gallagher aliyemzidi ujanja beki Victor Lindelof.

Kwa upande wake, bao la Fernandes ambaye ni raia wa Ureno lilichangiwa na difenda Luke Shaw katika dakika ya 44.

Man-United waliokuwa wakichezea ugenini walirejea uwanjani kwa minajili ya kipindi cha pili kwa matao ya juu huku kiungo Scott McTominay na fowadi Mason Greenwood wakimpa kipa Sam Johnstone wa West Brom kibarua kigumu cha kupangua makombora yao.

Nusura West Brom wafungiwe bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Diagne aliyeshuhudia fataki yake ikizuiliwa na mwamba wa goli la Man-United.

Licha ya sare, West Brom wangali katika hatari ya kuteremshwa ngazi kwenye kampeni za EPL msimu huu ikizingatiwa kwamba wanashikilia nafasi ya 19 kwa alama 13, mbili pekee mbele ya Sheffield United wanaovuta mkia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

AKILIMALI: Mwanafunzi wa JKUAT avuna hela kwa kukuza...

Askofu asema corona imewapa Wakenya fursa ya kumtambua Mola