• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Winga wa kupanda na kushuka Paul Were sasa mali ya Rayon nchini Rwanda

Winga wa kupanda na kushuka Paul Were sasa mali ya Rayon nchini Rwanda

NA GEOFFREY ANENE

WINGA wa kimataifa wa Kenya, Paul Were ameahidi makubwa waajiri wake wapya Rayon Sports nchini Rwanda.

Wakati wa kuzinduliwa kwake, Were, ambaye alinyakuliwa na miamba hao mnamo Agosti 11, alisema, “Nimejaa ari ya kutoa huduma zangu bora kabisa, kuonyesha kile naweza, kucheza na wachezaji wenzangu na kunyakua mataji kadha.”

Mchezaji huyo wa zamani wa akademia ya FISA, Mathare Youth, Tusker FC, AFC Leopards, amewahi kusakata kabumbu nchini Afrika Kusini, Ugiriki na Kazakhstan.

“Nafurahi sana na nina hamu kubwa kuanza ukurasa mpya na changamoto mpya katika klabu ya Rayon Sports. Shukran sana kwa upendo na uungwaji mkono. Twende kazi sasa. Mungu juu ya yote,” alisema winga huyo wa pembeni kushoto.

Winga wa kimataifa wa Kenya, Paul Were (kushoto) ameahidi makubwa waajiri wake wapya Rayon Sports nchini Rwanda. PICHA | HISANI

Were, 28, alichezea Harambee Stars mara 30 kati ya Novemba 11 mwaka 2011 na Julai 2019 akipachika magoli matatu.

Alikuwa katika kikosi cha kocha Sebastien Migne kilichoshiriki Kombe la Afrika 2019 nchini Misri, ingawa aliwekwa kitini katika mechi zote tatu Kenya ikibanduliwa katika awamu ya makundi.

Mechi ya kwanza ya Were huenda ikawa ile ya kufungua Ligi Kuu ya msimu 2022-2023 dhidi ya Rutsiro mnamo Agosti 20.

  • Tags

You can share this post!

Ruweida aweka historia akichukua kiti cha ubunge

Amri waliozua hofu kura zikijumlishwa Mavoko wakamatwe

T L