• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Yazamia kustawisha akademia ya soka kwa vizazi vijavyo

Yazamia kustawisha akademia ya soka kwa vizazi vijavyo

Na PATRICK KILAVUKA

Hillside FC imekuwa kitovu cha kuwezesha vipawa vya soka kukuzwa katika eneo la Ngong, kaunti ndogo ya Kajiado kaskazini ambako inapatikana uga wa Ngong Stadium.

Japo ilianzishwa miongo mitatu iliyopita, timu meneja wa sasa Josephat Namatsi anasema miaka ya awali, wachezaji walikuwa wanacheza tu kujijenga kiafya na kuchangamka. Kwa vile boli sasa imekuwa kazi, wanasoka wamekuwa wakisaka majani mabichi katika timu za mjini Nairobi kama njia ya kujitanua kisoka na kudumisha mikakati ya kujitafutia.

Na, hali hii imekuwa ikiiachia timu kovu la kuanza kujengwa upya. Imejitegemea kwa kipindi hicho huku ikijitahidi kujipiga jeki kushiriki Ligi ya Kauntindogo ya Kajido North.

Ni baada ya kuonesha ubabe wao katika Ligi hiyo na kuongoza msimu wa 2018, ilizamia kupiga shughuli katika Ligi ya Kauntindogo ya FKF, Nairobi West mwaka 2019 kuwapa wachezaji wake jukwaa la kushiriki Ligi yenye ushindani ya Kaunti ya Nairobi.

“Tumekuwa na lengo la timu kupata jukwaa la kujitanua na wanasoka kusajiliwa na timu za ligi za juu,” asema timu meneja huyo ambaye ameshirikiana sako kwa bako na kocha Oliver Obeoh ” Malo” na Ezekiel Saitoti aliye mwekahazina kusukuma gurudumu la timu hii.

Msimu huo, ilimaliza kileleni na kupanda ngazi msimu wa 2020-2021, Ligi ya Kaunti ya FKF, Nairobi West ambapo imejitahidi kukwea ligini japo ufadhili bado ungali kisiki.

“Ni kujitolea kwa wadau na baadhi ya wachezaji tumehakikisha dau letu la kupeperusha bendera ya timu ligini linatimia,” anasema timu meneja huyo ambaye ameongoza timu hadi ikamiliki nafasi ya 12 msimuni, ukiwa wa kwanza kushiriki.

Anaongezea kwamba, mipango ya timu ni kuwa kiota cha akademia ya soka kuivisha talanta,kuendela kutoa ushauri nasaha, kusajili mashabiki na kuendelea kusakata boli safi na tamanifu. Isitoshe, kusajiliwa wanadimba wa kuanzia chini ya miaka kumi kufungua mipango ya akademia.

Wadau wa timu wanayo mikakati ya kustawisha miradi ya vikundi kuwafanya wachezaji wamakinike zaidi mazoezi. “Timu ikiwa na miradi, wachezaji watakuwa na fursa ya kuhudhuria mazoezi bila changamoto nyingi na itakuwa imara zaidi,” wasema washikadau.

Imewahi kushiriki Chapa Dimba na kufika fainali ambapo ilibanduliwa na Laiser Hill Academy 2019. Isitoshe, 2016 ilicheza katika dimba la Alhali na kufika fainali. Matamanio yao sasa ni kucheza kwa bidii ili, timu iwe ya kwanza kuwakilisha Kaunti ya Kajido Kaskazini kwenye Ligi ya Kitaifa Daraja ya Kwanza, Ligi ya Supa (NSL) na hata kuingia Ligi Kuu majaliwa.

You can share this post!

KIPWANI: Dogo anayetikisa visiwa vya Lamu

20 waingia KCB Thika Rally inayofanyika wikendi hii

T L