• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Anataka tu kura, hana haja na maslahi ya wananchi, Mbadi amkashifu Ruto

Anataka tu kura, hana haja na maslahi ya wananchi, Mbadi amkashifu Ruto

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wachache Bungeni John Mbadi amemshtumu Naibu Rais William Ruto kuwa kuwahadaa Wakenya kwamba anajali maslahi yao kwa kupendekeza kuangusha Mswada wa Fedha 2022.

Akiongea na wanahabari Jumatano afisini mwake katika majengo ya bunge, mbunge huyo wa Suba Kusini alisema kuwa Dkt Ruto hazingatii ukweli, anapinga mswada huo kwani nia yake ni kuvuna kura za urais.

“Ruto anajifanya kuwa anajali masilahi ya Wakenya, kwa sababu anataka kura zao ili kufanikisha ndoto zake za kuwa rais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Huu ni unafiki mkubwa,” Bw Mbadi ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM, akasema.

Bw Mbadi alidai kuwa mnamo mwaka 2014, Dkt Ruto aliwatia shime wabunge wa Jubilee kupitisha pendekezo la sheria ya utozaji wa ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kwa bidhaa za kimsingi.

“Ruto na Aden Duale ambaye alikuwa kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa walitumia wingi wa wabunge wa Jubilee na kupitisha sheria ya VAT ambayo ilipandisha ushuru kwa bidhaa za kimsingi kama vile unga. Sasa ni unafiki kwa Naibu Rais kugeuzi kupinga mapendekezo ya kwenye mswada wa Fedha sawa na yale ambayo aliunga mnamo mnamo 2014,” akasema.

Mbunge Mbadi alisema ni yeye kama mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, ambaye alizuia utekelezaji wa ushuru huo wa VAT kwa bidhaa za chakula kwa kuomba Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi asitishe kuwasilisha mswada huo kwa Rais ili wabunge waiangalie upya.

Mnamo Jumapili Dkt Ruto, akiongea katika eneo la Banana kaunti ya Kiambu, aliapa kuwashawishi wabunge wandani wake kuangusha Mswada wa Fedha uliowasilishwa na bungeni na Waziri wa Fedha Ukur Yatani, muda mfupi kabla ya kusoma bajeti.

Naibu Rais alisema ni makosa kwa Waziri Yatani kupendekeza kutoza VAT kwa unga wa mahindi, unga wa ngano, unga wa muhogo na maji ya chupa ilhali Wakenya wanakabiliwa na ugumu wa maisha.

Hali hiyo imesababishwa na ukame, kupanda kwa bei ya mafuta, kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya miongoni mwa sababu nyinginezo.

Waziri Yatani pia amependekeza nyongeza ya ushuru utakaotozwa pikipiki za bodaboda, kuanzia Julai 1, 2022.

“Mswada huo na bajeti iliyosomwa bungeni itapandisha bei za maji, mkate, unga wa mahindi na pikipiki. Ningetaka kuwahakikishia hao watu kwamba bajeti hiyo na mswada wa fedha haitapita bunge. Na ikipita, tutawasilisha bajeti ya ziada miezi mitatu baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ili kupunguza bei ya bidhaa za kimsingi,” Dkt Ruto akasema, huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Mnamo Jumatano, hata hivyo Mbadi pia alisema kuwa tayari mrengo wao umewaagiza wabunge wao ambao ni wanachama wa Kamati ya Fedha kuondoa mapendekezo yanayoweza kuchochea ongezeko la bei ya bidhaa za kimsingi.

  • Tags

You can share this post!

Wafanyakazi wa Kenya Power motoni kwa wizi wa vifaa

Mahakama ya Rufaa sasa yairuhusu IEBC kutoa zabuni ya...

T L