• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Atwoli abashiri Raila atabwaga Ruto debeni

Atwoli abashiri Raila atabwaga Ruto debeni

NA SHABAN MAKOKHA

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Francis Atwoli amewataka wakazi wa Magharibi mwa Kenya waendelee kumuunga mkono kinara wa ODM, Raila Odinga, akisema ana imani atashinda kiti cha urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Bw Atwoli alisema kuwa idadi ndogo ya wapigakura waliojitokeza katika mchujo wa UDA mnamo Aprili 14 ni ishara kuwa Naibu Rais, Dkt William Ruto hana wafuasi na kwamba atapoteza urais kwa Bw Odinga.

Bw Atwoli alikariri kuwa idadi ndogo ya waliojitokeza kwenye mchujo wa UDA hasa katika eneo la Mlima Kenya inadhihirisha kuwa Naibu Rais ana wafuasi wachache “ilhali amekuwa akijidai ana wafuasi wengi” kutokana na idadi kubwa ya watu wanaojitokeza katika mikutano yake ya kisiasa.

Aidha, katibu huyo wa Cotu alidai kuwa Dkt Ruto hatapata kura nyingi eneo la Kati jinsi ambavyo imekuwa ikidaiwa kutokana na uhasama kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

“Wakazi wa Mlima Kenya wamekataa kumuunga mkono Ruto kutokana na matamshi makali ambayo amekuwa akimwelekezea Rais. Wamekerwa na kauli za Ruto na hawataki siasa zake tena,” akasema.

Bw Atwoli alikuwa akizungumza katika eneobunge la Khwisero wakati wa mazishi ya Herman Okeno, Jumamosi.

Kwa mujibu wa Bw Atwoli, Bw Odinga yuko kifua mbele katika kinyang’anyiro cha urais kwa kuwa ana uungwaji katika maeneo ya Magharibi, Pwani, Nairobi, Nyanza, Kati na Mashariki.

“Ruto anafikiria atapata kura wapi za kumshinda Raila Odinga? Hata katika Bonde la Ufa, huenda Raila akapata kura nyingi kumzidi,” akaongeza.

Alikariri kuwa Dkt Ruto hana uungwaji mkono wowote Magharibi akisema Kinara wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula walijiunga na mrengo wa Kenya Kwanza kama wanasiasa binafsi.

Alisema idhibati kuwa Mabw Mudavadi na Wetang’ula walienda Kenya Kwanza kivyao ni viongozi wachache ambao walihama nao kutoka Magharibi.

Aidha alimkashifu Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa kutoa masharti makali kwa Bw Odinga wakati anapoendelea kumfanyia kampeni maeneo mbalimbali nchini.

  • Tags

You can share this post!

Chelsea wadengua Palace na kujikatia tiketi ya kuvaana na...

Bodi ya filamu, KNDFF kushirikiana kukuza talanta

T L