• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Bahati itaendea nani?

Bahati itaendea nani?

MWANGI MUIRURI Na BENSON MATHEKA

SUALA la mgombea mwenza wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga katika Azimio la Umoja One Kenya Alliance linaendelea kupandisha joto katika muungano huo.

Eneo la Mlima Kenya linamsukuma Bw Odinga kuteua mgombea mwenza kutoka eneo hilo huku kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka akisisitiza kuwa ndiye anayetosha kuwa naibu wa Bw Odinga.

Makamu rais huyo wa zamani amekataa mbinu ya kuteua mgombea mwenza wa Bw Odinga kupitia kamati iliyosemekana kuteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Rais Kenyatta ndiye mwenyekiti wa Baraza la Azimio huku Bw Odinga akiwa kiongozi wa muungano huo.

Wanasiasa wa eneo hilo wanaounga muungano huo wanatumia kila mbinu kuhakikisha Bw Odinga atamteua aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth au kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake.

Haya yanajiri huku wachambuzi wa siasa wakikubaliana kuwa Bw Odinga anafaa kuteua mgombea mwenza kutoka eneo hilo au Mashariki ya chini anakotoka Bw Musyoka.

Kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap Alfred Mutua anayetoka Mashariki ya chini ya nchi pia anamezea mate wadhifa wa naibu wa Bw Odinga.

Japo Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe amewahi kunukuliwa akisema kwamba Bw Odinga atashinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 hata kama eneo la Kati halitampigia kura, baadhi ya wenzake wanasisitiza kuwa tamko hilo halina mashiko.

Bw Musyoka, Bw Kenneth na Bi Karua wamewahi kugombea urais na kura walizopata zinatumiwa kupima uwezekano wao kuteuliwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

“Bw Musyoka alipata kura 879,903 katika uchaguzi wa urais wa 2007 na amekuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga mara mbili ambapo waliibuka katika nafasi ya pili mwaka wa 2013 na 2017. Kwa kuzingatia haya, Musyoka ndiye anafaa kuwa mgombea mwenza,” anasema mchanganuzi wa siasa za eneo la Mlima Kenya Profesa Ngugi Njoroge.

Anaongeza kwamba Bw Kenneth alipata kura 72,000 huku Bi Karua akipata kura 43,000 kwenye uchaguzi wa urais wa 2013. Washirika wa Rais Uhuru Kenyatta wanasisitiza kuwa chama chao cha Jubilee na ODM cha Bw Odinga ndivyo vikubwa katika Azimio na kwa hivyo, wadhifa wa mgombea mwenza unafaa kutoka eneo lao.

Bw Kenneth anasema kwamba “vinara wa Azimio la Umoja ni Rais na Bw Odinga na ni wazi anakofaa kutoka mgombea mwenza.”

Anasema kwamba mito mikubwa haijiungi na ile midogo na kwa hivyo Mlima Kenya na idadi kubwa ya wapigakura katika eneo hilo inafaa kuzingatiwa wakati wa kuchagua mgombea mwenza wa Bw Odinga.

Kulingana na mdadisi wa siasa Keith Wariara, Bi Karua anastahili wadhifa huo ili kuleta usawa wa jinsia katika Azimio la Umoja One Kenya.

“Bw Odinga akizingatia idadi ya wapiga kura wanawake katika nchi, anafaa kumteua Bi Karua kuwa mgombea mwenza wake,” alisema.

Hata hivyo Bi Karua anasisitiza kuwa anagombea ugavana kaunti ya Kirinyaga.

Huku washirika wa Bw Musyoka wakisisitiza kuwa makamu rais huyo wa zamani ni lazima awe mgombea mwenza wa Bw Odinga, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni anasema kwamba “muundo wa serikali ijayo una Bw Odinga kama mgombea urais na wengine ni Wakenya wa nia njema.”

Msemaji wa Azimio na mwanamikakati wa Bw Odinga anasema kwamba mgombea mwenza anafaa kuwa mtu anayeelewa majukumu ya ofisi hiyo, aliye na idadi kubwa ya kura na aliyedhihirisha uaminifu.

  • Tags

You can share this post!

Walimu wataja kiini cha shule kuchomwa

Mithika Linturi ateua mgombeaji mwenza

T L