• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
BBI kuwasilishwa bungeni kesho

BBI kuwasilishwa bungeni kesho

Na CHARLES WASONGA

MSWADA wa marekebisho ya Katiba kupitia mapendekezo ya jopo ya maridhiano (BBI) utawasilishwa rasmi katika Bunge la Kitaifa Alhamisi, Machi 4.

Spika wa bunge hilo Justin Muturi aliamuru kwamba mswada huo usomwe kwa mara ya kwanza katika kikao cha bunge lote ili wabunge waanze kuuchanganua.

“Nimeamuru karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai kuwatoa nakala za kutosha za mswada huo ili ziweweze kusambazwa kwa wabunge wote 349 wausome. Hii itawawezesha kuweza kushiriki mjadala kuuhusu katika awamu ya mjadala kuhusu mswada huo,” Bw Muturi akawaarifu wabunge katika kikao cha jioni Jumanne.

Bw Muturi alipuuzilia mbali pendekezo la baadhi ya wabunge wa mrengo wa Tangatanga wakiongozwa na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale waliotaka mswada huo ulipokewa kutoka mabunge ya kaunti uandikiwe upya kabla ya kushughulikiwa na wabunge.

“Naamuru kuwa nakala ambazo zitasambaziwa wabunge zitakuwa sawa na mswada ambao uliwasilishwa katika mabunge 47 na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Bunge halina mamlaka ya kuubadilisha au kuufanyia marekebisho mswada huo,” akasema Bw Muturi.

Kulingana na kipengele cha 257 cha Katiba kuhusu mageuzi ya katiba kupitia ushirikishwaji wa wananchi (popular initiative) Bunge la Kitaifa na lile la Seneti hayana mamlaka ya kuufanya marekebisho yoyote mswada wa marekebisho ya katiba baada ya kupitishwa na angalau mabunge 24 ya kaunti.

Isitoshe, baada ya mswada huo kupitishwa na idadi hiyo ya mabunge ya kaunti, maamuzi ya bunge la kitaifa na seneti kuuhusu hayatazuia kufanyika kwa kura ya maamuzi. Hii ina maana kuwa hata kama mabunge hayo mawili yataupinga Mswada huo wa BBI, bado Wakenya watapata nafasi ya kushiriki kura ya maamuzi kuuidhinisha au kuukataa.

Kufikia Jumanne, jumla ya mabunge 43 ya kaunti yalikuwa yamepitisha maswada huo huku mabunge Baringo, Nandi na Elgeyo Marakwet yakiwa ya kipekee yaliyopinga.

Siku hiyo bunge la kaunti ya Mandera lilikuwa la 43 kupitisha mswada huo baada ya madiwani 34 kupiga kura ya NDIO, mmoja kupinga na wengine 13 hawakushiriki upigaji kura.

Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu ndilo la kipekee ambalo halijaujadili na kuupigia kura mswada huo.

Mnamo Februari 25, Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wakuu wa vyama mbalimbali vya kisiasa wakutana katika Ikulu ya Nairobi ambapo walitoa taarifa ya pamoja kuwapongeza madiwani wa kaunti zilizoidhinishwa mswada huo.

Viongozi hao walikuwa pamoja na, Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Gideon Moi (Kanu) na Gavana wa Kitui Charity Ngilu (Narc).

Saba hao walitoa wito kwa Wakenya kuunga mkono mpango huo wa marekebisho ya katiba wakisema yanalenga kushughulikia changamoto kadha yanayowasibu.

“Leo, kwa niaba ya taifa letu tukufu, tunatoa shukrani zetu kwa mabunge yote ya kaunti kwa kuunga mkono mchakato huu. Hatua yao imeweka msingi ambapo Kenya itaendeleza azma ya kufikai usawa katika ugavi wa rasilimali, usawa wa kijinsia, hakikisho la usawa katika ugavi wa nafasi kwa wa rasilimali ambapo kile Mkenya atapata sehemu ya amali ya nchi,” Seneta Moi akasema kwenye taarifa ya pamoja aliyosoma kwa niaba ya wenzake sita.

Viongozi hao wa vyama waliahidi kuendelea michakato ya uhasisho wa umma kuhusu manufaa ya mswada wa BBI.

Mnamo Jumanne Spika Muturi alisema kuwa baada ya mswada huo kuwasilishwa rasmi katika bunge la kitaifa utapitishwa kwa Kamati kuhusu Haki na Masuala ya Sheria ambayo itaandaa vikao vya kukusanya maoni ya umma kuuhusu.

“Nataraji kuwa Kamati hiyo itafanya kazi hiyo haraka na kisha kuwasilisha ripoti yake katika kikao cha bunge lote inajadiliwe na kupigiwa kura. Hii ni kazi ambayo itachukua muda wa majuma mawili au matatu. Hatutarajii kutumia muda wa siku 90 kama ilivyo kawaida,” akasema Bw Muturi.

You can share this post!

Shehena ya chanjo ya corona yafika Kenya

Udikteta ulivyolemaza vita dhidi ya corona Tanzania