• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
CCM yakataa kuingia UDA

CCM yakataa kuingia UDA

Na FRED KIBOR

HATUA ya Naibu Rais Dkt William Ruto ya kutaka vyama vyote vinavyounga mkono azma yake ya kuingia ikuluni 2022 vivunjwe kisha vijiunge na UDA, imekashifiwa na Chama cha Mashinani (CCM) ambacho kinaongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto.

Licha ya kuwa CCM imesema kuwa inaunga mkono azma ya Urais wa Dkt Ruto, chama hicho kimesisitiza kuwa hakitavunjwa na kitawasilisha wawaniaji wa nafasi nyingine za uongozi isipokuwa ile ya urais pekee.

Kaimu Katibu Mkuu wa CCM Albert Kochei jana aliambia Taifa Leo kuwa uongozi wa chama hicho ulikutana na kuafikiana kuwa watawasilisha wagombeaji katika vyeo vingine vya uongozi mnamo 2022.

“Mwaniaji ambaye tunamvumisha 2022 anasalia kuwa Naibu Rais Dkt Ruto. Kama chama tutapigania viti vingine wala hatutaingia kwenye mkataba wa ushirikiano na chama chochote hata UDA. CCM inasimamia demokrasia, usawa na uhuru wa Wakenya,” akasema Bw Kochei.

Katibu huyo alishikilia kuwa haitakuwa sawa iwapo baadhi ya wanasiasa watawashurutisha wenzao wavunje vyama vyao, akisema hatua hiyo ni kurejesha taifa katika enzi za utawala wa chama kimoja.

“Tunamuunga mkono Dkt Ruto kwa sababu kauli mbiu yake ya hustler inawiana na ajenda ya CCM. Sote tunapigania usawa na kuinuliwa kwa maisha ya Mkenya wa kawaida,” akaongeza.

Alisema CCM ilichukua msimamo huo kutokana na kile ambacho kilitokea baada ya kuvunjwa kwa chama cha Jubilee, alichodai kuwa sasa kimesalia kama kigae.

“Wakenya wamejifunza kutokana na kile ambacho kilifanyika ndani ya Jubilee na raia nao wanatumia vyama ili kuhakikisha viongozi wanawawajibikia. Vyama vya kisiasa huwa ni maarufu sana wakati wa uchaguzi kwa sababu ni kutokana na uwepo wao ambapo raia wapo hiari kuwachagua viongozi bora.”

Aidha, Bw Kochei alisema chama hicho pia hakitawapokea wawaniaji ambao wamehama vyama vyao baada ya kulemewa katika uteuzi wa tiketi hata iwapo watatokea UDA au chama chochote kingine.

“Sisi tunaongozwa na sheria na wale ambao wana manifesto inayoshabikiwa na raia ndio watatumia tiketi yetu,” akasisitiza.Katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wanasiasa wengi wandani wa Dkt Ruto wanapigania kutwaa tiketi ya UDA huku suala kuu likiwa.; iwapo kutakuwa na uwazi katika shughuli za uteuzi.

“Iwapo uteuzi utavurugwa basi UDA itapoteza umaarufu hali ambayo haifai kutokea. Uteuzi unafaa uwe wazi na wandani wa Dkt Ruto hawafai kutumia ukuruba wao kupata tiketi za moja kwa moja,” akasema Jonathan Bii, anayelenga kiti cha Ugavana cha Uasin Gishu.

Hata hivyo, Mshirikishaji wa UDA Uasin Gishu Paul Kiprop aliwahakikishia wote kuwa uteuzi huo utakuwa huru.

“Kiongozi wetu amezungumzia suala hili mara kadhaa na akatuhakikishia kuwa kila mwaniaji atakuwa na nafasi ya kupigania tiketi debeni. Katika ngome za UDA hatutavumilia tabia ya watu kuidhinishwa na kulazimishiwa raia kwa sababu wawaniaji wote ni sawa,” akasema Bw Kiprop.

You can share this post!

Mjumbe wa Taliban anyimwa fursa kuhutubia kikao cha UN

Miswada yataka walioshtakiwa wasiwanie viti