• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
China ilivyomfunga Uhuru mdomo

China ilivyomfunga Uhuru mdomo

PAUL WAFULA Na VINCENT ACHUKA

CHINA ilizuia Rais Uhuru Kenyatta kutangazia Wakenya yaliyomo kwenye kandarasi ya ujenzi wa reli ya SGR kama alivyoahidi kwa kuweka masharti makali ya utoaji habari kuhusu mradi huo.

Hii ni baada ya kampuni ya China iliyoweka kandarasi ya ujenzi huo na Kenya kukataa kukubali kandarasi hiyo kutangaziwa umma kutokana na kifungu kinachotaka iwekwe siri kubwa.

Miezi 13 iliyopita, Rais Kenyatta aliahidi kutangazia Wakenya yaliyomo kwenye kandarasi hiyo, lakini kufikia sasa hajatimiza ahadi yake.

Imefahamika kuwa baada ya kutoa ahadi hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na Wizara ya Uchukuzi walishauri dhidi ya kutolewa kwa kandarasi hiyo kwa umma kutokana na kifungu ambacho kinataka iwekwe siri.

Hii imeibua maswali ya sababu ya kandarasi ya mradi wa umma kuwekwa siri kubwa licha ya kugharamiwa na walipa ushuru Wakenya.

Baada ya kugundua Kenya ilichezewa katika kandarasi hiyo, maafisa wa serikali walijaribu kuijadili upya ili kuondoa vifungu vinavyonyanyasa Kenya, lakini wakagonga mwamba.

Hii ni baada ya kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC) kukataa kutoa habari hizo ikitaja kuwa inafaa kubakia siri kubwa.

Kandarasi hiyo ambayo Taifa Leo ilipata kusoma inasema lazima pande mbili husika ziweke sahihi makubaliano ya kutolewa kwa ripoti hiyo kwa umma.

Kifungu hicho ndicho kilimfanya Rais wa Jamhuri ya Kenya kufungwa mikono katika juhudi za kuwaeleza raia wake yaliyomo kwenye kandarasi hiyo.

Kulingana na kandarasi hiyo, mabilioni ya pesa yalitumika kwa manufaa ya China.

Hii ilikuwa ni katika uajiri wa wafanyikazi wengi kutoka China kufanya kazi ambazo Wakenya wangeweza kutekeleza, Wachina kulipwa mishahara na marupurupu makubwa kuliko Wakenya, vifaa kuingizwa nchini bila kutozwa ushuru na bei ya vifaa kuwa ya juu kupindukia.

Gharama hizo za juu za SGR ya Kenya zilifanya igharimu Sh335 bilioni kujenga kilomita 472 kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Hii ni gharama ya juu kupindukia ikizingatiwa Tanzania inajenga SGR ya umbali wa kilomita 422 kwa gharama ya Sh192 bilioni, ambapo treni zake zitakuwa zikitumia stima kinyume na za Kenya ambazo zinatumia dizeli.

Kulingana na ripoti hiyo, Wachina 5,795 waliletwa nchini kufanya kazi katika ujenzi wa SGR, ajira ambazo zingefanywa na Wakenya.

Wachina hao pia walilipwa mishahara ya juu na marupurupu kuliko Wakenya ambao walikuwa wakifanya kazi sawa na wao.

Wachina hao pia walipewa nyumba zilizopambwa na pia wafanyikazi wa nyumbani.

Pia walilipwa marupurupu ya ziada kwa kufanya kazi baada ya muda wa kawaida huku Wakenya wakiambulia patupu.

Kati ya wafanyikazi 5,795 waliotoka China, 95 pekee ndio waliokuwa wataalamu huku wengine 5700 wakifanya kazi ambazo zingetekelezwa na Wakenya kama vile kuendesha malori, trakta na mashine zingine za ujenzi.

Kampuni hiyo wakati huo ilidai kuwapa Wakenya 19,858 kazi, lakini stakabadhi zake hazina habari hizo.

Hii huenda ikatokana na kuwa kandarasi za uajiri wa Wakenya zilikuwa na dosari.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Sh1.3 bilioni zilitumika kugharamia mahitaji ya wahadisi watano wakuu wa mradi huo zikiwemo Sh72 milioni za kulipa wafanyikazi wa nyumbani.

Wakenya ambao waliajiriwa kufanya kazi hizo za nyumbani walilipwa kati ya Sh3,580 na Sh12,274.

Ripoti hiyo pia inaeleza kwamba zaidi ya Sh1 bilioni zilitumika kupanda nyasi kando ya reli hiyo.

Bei za vifaa nayo ilipandishwa kupindukia. Kwa mfano mashine ya kuchomelea inayouzwa Sh25,000 iligharimu Sh442,000, basi ndogo la Sh1.5 milioni likauzwa Sh12 milioni nayo mashine ya kupiga chapa ikauzwa Sh500,000 badala ya Sh75,000.

You can share this post!

AKILIMALI: Ifahamu mikate ya ng’ombe kutoka Kalro

Utwaaji wa serikali ya Nairobi huenda usilete nafuu

adminleo