• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
CPK yabaki kwa mataa baada ya Mwadime kuhama

CPK yabaki kwa mataa baada ya Mwadime kuhama

NA LUCY MKANYIKA

CHAMA cha Communist Party of Kenya (CPK) kimemkosoa Mbunge wa Mwatate, Bw Andrew Mwadime, kukihama dakika za mwisho na hivyo kukiacha bila mgombea ugavana Taita Taveta.

Bw Mwadime ambaye amepanga kuwania ugavana Taita Taveta katika uchaguzi wa Agosti alikuwa amehamia chama hicho Aprili kwa kuhofia kuwa chama chake cha ODM kingempa Gavana Granton Samboja tikiti ya moja kwa moja kutetea kiti chake.

Hata hivyo, Bw Samboja alikabidhiwa tikiti na chama cha Jubilee.

“Angetuambia mapema ili tutafute mgombeaji mwingine. Tulimpa tikiti lakini akajiondoa dakika za mwisho. Kwani alikuwa ametumwa kuvuruga chama chetu?” akalalamika mwenyekiti wa CPK, Bw Mwandawiro Mghanga.

Juhudi za kumfikia Bw Mwadime kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba, lakini wandani wake walisema alifanya uamuzi huo kwa vile CPK iliamua kushirikiana na Naibu Rais, Dkt William Ruto kisiasa.

Duru zilisema mbunge huyo ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka wa 2013 aliamua atawania ugavana kama mgombeaji huru kwa vile misimamo yake hailingani na ile ya Muungano wa Kenya Kwanza.

Bw Mwadime anatarajiwa kushindania ugavana dhidi ya Bw Samboja, aliyekuwa gavana John Mruttu (UDA), aliyekuwa seneta Dan Mwazo (Wiper), Thomas Mwakwida (ODM), Patience Nyange (Narc-Kenya), miongoni mwa wengine.

CPK itakuwa na wagombeaji viti tofauti zaidi ya 30 katika Kaunti ya Taita Taveta na kaunti nyingine za Pwani, ambapo Bw Mghanga atawania useneta dhidi ya Bw Jones Mwaruma.

You can share this post!

Gavana ashauri wakazi kutumia vyema mikopo

Liverpool yadengua Villarreal ya Uhispania na kutinga...

T L