• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Liverpool yadengua Villarreal ya Uhispania na kutinga fainali ya UEFA

Liverpool yadengua Villarreal ya Uhispania na kutinga fainali ya UEFA

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL watakutana na Manchester City au Real Madrid kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayochezewa mnamo Mei 28, 2022 jijini Paris, Ufaransa msimu huu.

Itakuwa mara ya tatu katika kipindi cha misimu mitano iliyopita kwa masogora hao kunogesha fainali ya kipute hicho. Liverpool walitoka chini kwa mabao 2-0 na kupepeta Villarreal 3-2 katika mkondo wa pili wa nusu-fainali mnamo Jumanne usiku nchini Uhispania.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, miamba hao wa soka ya Uingereza walijibwaga ugani kwa mchuano huo wa marudiano wakijivunia ushindi wa 2-0 ugani Anfield mnamo Aprili 27, 2022. Hivyo walisonga mbele kwa jumla ya mabao 5-2.

Ushindi wa Liverpool uliweka hai matumaini yao ya kuandikisha historia ya kuwa kikosi cha kwanza kutoka Uingereza kuwahi kujizolea jumla ya mataji manne katika kampeni za msimu mmoja.

Kufikia sasa, kikosi hicho kilichozoa taji la Carabao Cup mwishoni mwa Februari 2022, kinashikilia nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL kwa alama 82, moja pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Manchester City. Kitavaana na Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA ugani Wembley mnamo Mei 14, 2022.

Boulaye Dia aliweka Villarreal kifua mbele katika dakika ya tatu baada ya kushirikiana na Etienne Capoue aliyechangia bao la pili lililopachikwa wavuni na beki wa zamani wa Arsenal, Francis Coquelin.

Liverpool walirejea mchezoni katika kipindi cha pili kupitia kwa bao la Fabinho katika dakika ya 62 kabla ya nguvu mpya Luis Diaz aliyejaza nafasi ya Diogo Jota kumwacha hoi kipa Geronimo Rulli dakika tano baadaye.

Sadio Mane alifunga bao la tatu la Liverpool na kufikia rekodi ya Frank Lampard aliyewahi kupachika wavuni mabao 15 katika nusu-fainali za UEFA akivalia jezi za kikosi kinachoshiriki soka ya EPL, Chelsea.

Villarreal walikamilisha mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Capoue kuonyeshwa kadi nyekundu dakika tano kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo.

Hii ni mara ya 10 ambapo Liverpool wametinga fainali ya European Cup au UEFA na sasa wana motisha ya kutawazwa wafalme wa bara Ulaya kwa mara ya saba baada ya kutwaa mataji ya 1977, 1978, 1981, 1984, 2005 na 2019.

Iwapo Real watabatilisha kichapo cha 4-3 walichopokezwa na Man-City kwenye mkondo wa kwanza wa nusu-fainali nyingine ya UEFA watakaporudiana mnamo Mei 4, 2022, basi watarejesha kumbukumbu ya fainali ya 2018 ambapo walizamisha Liverpool 3-1 jijini Kyiv, Ukraine.

Liverpool ambao ni mabingwa hao mara 19 wa EPL, watakuwa wenyeji wa Tottenham Hotspur ligini mnamo Mei 7, 2022 kabla ya kuendea Aston Villa kisha kufunga kampeni za EPL dhidi ya Southampton na Wolves kwa usanjari huo.

Tofauti na Villarreal waliopigwa 2-1 na Alaves wikendi iliyopita katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Liverpool walijitosa ulingoni mnamo Jumanne usiku wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Newcastle United katika pambano la awali la EPL.

Ushindi dhidi ya Newcastle uliwakweza Liverpool kileleni mwa jedwali la EPL kwa saa chache kabla ya mabingwa Man-City kuponda Leeds United 4-0 uwanjani Elland Road na kurejea uongozini.

Liverpool walijitosa ugani La Ceramica wakipigiwa upatu wa kuteremkia Villarreal licha ya Juventus na Bayern Munich kushindwa kuangusha masogora wa Emery katika UEFA ugani humo muhula huu. Hata hivyo, Villarreal hawakuwa wamepoteza mechi yoyote kati ya 12 za awali katika uwanja wao wa nyumbani tangu Novemba 2021.

Ni kikosi kimoja pekee ambacho kimewahi kubatilisha kichapo cha zaidi ya mabao mawili kwenye nusu-fainali ya UEFA na kutinga fainali. Klabu hiyo ni Liverpool iliyopepeta Barcelona 4-0 katika marudiano licha ya kupoteza mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya 2018-19 kwa 3-0.

Iwapo Liverpool sasa wamo katika kundi moja na Real (16), Bayern (11) na AC Milan (11) ambao wamewahi kunogesha fainali ya kivumbi hicho zaidi ya mara 10.

Mchuano dhidi ya Villarreal ulikuwa wa sita mfululizo kwa Liverpool kushinda katika mashindano yote. Walikamilisha mechi nne kati ya tano za awali bila kufungwa bao na hawajahi kupoteza pambano lolote ugenini tangu Disemba 2021 Leicester City iwakung’ute 1-0 ugani King Power.

Rekodi hiyo imewashuhudia wakishinda michuano yote sita ya ugenini katika UEFA msimu huu huku wakifunga angalau mabao mawili katika kila mojawapo ya mechi hizo. Liverpool walipigwa 1-0 walipokutana na Villarreal mara ya mwisho ugani La Ceramica kwenye nusu-fainali ya Europa League mnamo 2015-16.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

CPK yabaki kwa mataa baada ya Mwadime kuhama

Ni Nassir vs Sonko kivumbi Mombasa kukabana koo –...

T L