• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Duale awaongoza wabunge wa ‘Tangatanga’ kuondoka kwenye kikao cha JLAC

Duale awaongoza wabunge wa ‘Tangatanga’ kuondoka kwenye kikao cha JLAC

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa mrengo wa Tangatanga Jumanne, Desemba 28, 2021 walioondoka kwa hasira kutoka kwenye kikao cha Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) wakipinga uwepo wa wadau wengine ambao sio wabunge.

Wakiongozwa na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale, Kimani Ichungwa (Kikuyu), Alice Wahome (Kandara), Didmus Barasa (Kimilili), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Daniel Tuitoek (Mogotio), John Mutunga (Tigania Mashariki) na Mbunge wa Kipkelion Mashariki Joseph Limo, walipinga uwepo wa Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ROPP) Anne Nderitu, Mwenyekiti wa Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT), miongoni mwa wengine.

Mkutano huo ambao ulifanyika katika ukumbi wa County Hall katika majengo ya bunge, Nairobi uliitishwa kuoanisha mabadiliko 17 yaliyopendekezwa kwa Mswada wa Mabadiliko ya Sheria za Vyama vya Kisiasa.

Mabadiliko hayo yalipendekezwa katika kikao maalum cha bunge la kitaifa kilichofanyika mnamo Desemba 22, 2021.

Naibu Spika Moses Cheboi alipendekeza kwamba kamati hiyo ya JLAC chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Kangema Muturi Kigano, ioanishe mapendekezo hayo kisha iwasilishe ripoti katika kikao kijacho cha bunge. Hapo ndipo akaahirisha kikao hicho maalum hadi wakati huo.

Lakini siku moja baadaye, mnamo Desemba 23, 2021, Spika Muturi aliitisha kikao kingine maalum ili kushughulikia mswada huo mnamo Jumatano, Desemba 29, 2021.

Kwenye taarifa iliyochapishwa katika toleo maalum la gazeti rasmi la serikali, Bw Muturi alisema kuwa wabunge wanaweza kufanya kikao cha usiku endapo kufikia jioni hawatakuwa wamemaliza kushughulikia mswada huo.

Kabla ya kuondoka kutoka kikao hicho Bw Duale alikuwa na cha kusema.

“Siwezi kuwasilisha mapendekezo yangu kuhusu mswada huu mbele ya baadhi ya maafisa ambao napendekeza kwamba mamlaka yao yapunguzwe,” akasema Bw Duale.

Mbunge wa Kandara naye alikuwa na jambo.

“Nilifika hapa kama Mbunge mwenye haki ya kuwasilisha mabadiliko katika mswada. Kwa hivyo, sio vizuri kwangu kuketi katika mkutano mmoja na wadau ambao hawana mamlaka ya kutengeneza sheria. Kwa kufanya hivyo, sitakuwa nikitelekeza wajibu wangu kama mbunge. JLAC ingeketi kwanza na kukamilisha kikao cha kukusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu mswada huu, kabla ya kuwaita wabunge kwa kikao cha kuoanisha hoja za mageuzi,” akasema Bi Wahome.

Mabw Barasa, Baya, Tuitoek na Dkt Mutunga pia waliondoka kwa misingi hiyo hiyo.

“Ni makosa kwa kamati hii kumwalika Msajili wa Vyama vya kisiasa katika mkutano huu ilhali nimependekeza mageuzi ya kudhibiti kuhusishwa kwa afisi yake katika michujo ya vyama vya kisiasa. Je, atatetea hoja hiyo akiwa hapa?” Bw Barasa akauliza.

  • Tags

You can share this post!

Namna ufalme wa Mwendwa katika soka nchini ulivyoporomoshwa...

Viongozi zaidi, wazee wapinga mkutano wa Atwoli Ijumaa

T L