• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Namna ufalme wa Mwendwa katika soka nchini ulivyoporomoshwa na mkono mrefu wa serikali

Namna ufalme wa Mwendwa katika soka nchini ulivyoporomoshwa na mkono mrefu wa serikali

Na CECIL ODONGO

MNAMO Novemba 4, 2006 aliyekuwa Waziri wa Michezo Maina Kamanda alivunja lililokuwa wakati huo Shirikisho la Soka Nchini (KFF) kutokana na malumbano kati ya kambi mbili pinzani.

Mwaka huo, mirengo miwili iliyokuwa ikiongozwa na Alfred Sambu (sasa mbunge wa Webuye Mashariki) na Mohammed Hatimy (sasa marehemu) ililumbana kuhusu usimamizi wa Ligi Kuu Nchini.

Kamanda (sasa mbunge maalum) alivunja KFF na kuteua kamati ya muda ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mtana Lewa kusimamia soka kisha uchaguzi wa KFF ukaandaliwa baadaye.

Miaka 15 baadaye, matukio hayo ya 2006 yamejirudia nchini huku mchezo wa soka ukishuhudia malumbano na mabadiliko makubwa mwaka huu unaokamilika wa 2021.

Mwanzo, Waziri wa Michezo Amina Mohamed mnamo Novemba 11 alivunja Shirikisho la Soka Nchini (FKF) lililokuwa likiongozwa na Nick Mwendwa.

Waziri wa Michezo Amina Mohamed (kulia) akiwa na aliyekuwa Rais wa FKF Nick Mwendwa. PICHA | MAKTABA

Uhasama kati ya wawili hao ulikuwa umegonga vichwa vya habari huku Mwendwa wakati mmoja akinukuliwa akisema kuwa Mohamed hakufahamu hata mpira wa kona ni nini.

Hatua ya Mohammed kuvunja FKF ilichochewa na matokeo ya ripoti ya ukaguzi kwenye vitabu vya shirikisho hilo ambayo ilifichua kukithiri kwa ubadhirifu wa fedha zilizotolewa kufadhili timu za soka zilizokuwa zikiwakilisha taifa kwenye mashindano mbalimbali.

Amri kuwa ukaguzi huo ufanyike ilitolewa mnamo Oktoba 17 na Mohamed kwa Msajili wa Michezo Rose Wasike. Hata hivyo, Mwendwa na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF Barry Otieno waliupinga, wakihoji kuhusu nia ya serikali kwenye mchakato wa kuendesha uchunguzi huo.

Mara tu baada ya kuvunja FKF, Mohammed alilambisha kambi ya Mwendwa sakafu zaidi alipoteua kamati ya muda chini ya uongozi wa Jaji Mstaafu Aaron Ringera siku hiyo hiyo ya Novemba 11 kusimamia soka nchini.

Kando na Ringera, wanachama wengine wa kamati hiyo inayoendelea na kazi yake hadi sasa ni Meja Mstaafu Moses Oyugi, Fatma Adan, Philip Musyimi, Anthony Isayi, Elisha Kiplangat, Hassan Mahmoud Hajji, Fredrick Lekesike, Ali Amour, aliyekuwa Naibu Rais wa FKF Titus Kasuve, waliokuwa wakuu wa Chama cha Raga Nchini Mwangi Muthee na Richard Omwela, Kocha Mkuu Kenya Police John Bobby Ogolla, jagina wa AFC Leopards JJ Masiga na fowadi wa Harambee Starlets Neddy Atieno.

Sekretariati ya kusimamia ligi kuu, ile ya NSL, Ligi ya Wanawake ambazo zilisimamishwa kwa wiki tatu baada ya FKF kuvunjwa pia ilibuniwa na Mohammed. Mwanahabari Linda Ogutu aliteuliwa msimamizi mkuu akisaidiwa na Michael Muchemi na Loreen Shitubi kama makatibu wenza.

Wengine walioteuliwa kwenye sekretariati hiyo ni Caser Handa, Hiba Hussein, Gabriel Warigi, aliyekuwa mchezaji wa raga Edward Rombo, Dkt Walter Ongeti kutoka Wizara ya Michezo, aliyekuwa kocha wa KCB na Thika United Rishadi Shedu na Rachel Kamweru ambaye aliwahi kudumu kama mwanachama wa Baraza Kuu la FKF akiwakilisha ukanda wa Mashariki.

Ingawa FKF ilielekea kortini kupinga kubuniwa kwa kamati hiyo ikisema hatua ya Mohamed ilikuwa kinyume cha sheria, kesi hiyo bado ipo mahakamani na inatarajiwa kusikizwa mnamo Januari 17 ambapo tarehe ya uamuzi kutolewa itatangazwa.

Hatua ya Mohammed kuvunja FKF ilitokana na kubanduliwa kwa Kenya kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2022 ambapo Harambee Stars ilimaliza nafasi ya tatu kwenye kundi ambalo lilikuwa na majirani Uganda, Rwanda na Mali.

Kilio cha mashabiki wa soka kilitanda zaidi baada ya Kenya kucharazwa 5-0 na Mali kule Morocco mnamo Oktoba 8. Inakisiwa kuwa hiyo pia ilikuwa mojawapo ya sababu zilizomsukuma Mohamed kuvunja FKF. Awali Kenya ilikuwa pia imebanduliwa kwenye kipute cha kufuzu Mataifa Bingwa Afrika (AFCON) ambacho kitaandaliwa Cameroon mnamo Januari, 2022.

Baada ya kuvunjwa kwa FKF Novemba 11, Mwendwa aliitisha kikao na wanahabari katika hoteli ya Safari Park, na kumchemkia Mohamed akiapa kutobanduka huku tetesi zikienea kuwa Kenya ingepigwa marufuku kushiriki mashindano mbalimbali ya soka na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa kumfurusha Mwendwa.

Hata hivyo, kitumbua cha Mwendwa kilingia mchanga zaidi kwa kuwa afisi za FKF zilizoko Goal Project, Kasarani zilizingirwa na maafisa wa polisi na hakuna mfanyakazi wa shirikisho hilo ambaye aliruhusiwa kuingia humo.

Siku iliyofuata ya Novemba 12, Mwendwa alinyakwa na makachero wa DCI, akapelekwa katika kituo cha polisi cha Gigiri ambako alilala wikendi nzima kisha akapelekwa mahakamani Novemba 15.

Hata hivyo, hakushtakiwa huku upande wa mashtaka ukiomba muda zaidi wa kumzuilia ili kukamilisha uchunguzi. Aliwakilishwa na mawakili Eric Mutua na Tom Ojienda ambao waliwahi kuongoza Chama cha Mawakili Nchini (LSK) pamoja na mwenyekiti wa sasa Nelson Havi. Mawakili wengine waliomwakilisha walikuwa Senata Mutula Kilonzo Junior, Vincent Omwebu na Charles Njenga.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh7 milioni au Sh4 miloni pesa taslimu. Ingawa hivyo, mnamo Novemba 26, serikali ilikosa kuwasilisha mashtaka dhidi yake na Hakimu Mkuu Mkaazi wa Mahakama ya Mlimani Wandia Nyamu akafunga faili ya kesi yake na kuamuru arejeshewe dhamana yake.

Siku moja baadaye, Mwendwa alinyakwa tena, akaishia kwenye seli wikendi nzima ila alipofikishwa kortini mnamo Novemba 29 alikataa kujibu mashtaka akisema haki zake zilikiukwa kutokana na jinsi alivyobambwa.

Mnamo Novemba 30, alirejeshwa kortini ambapo alikanusha kuwa alipora Sh38 milioni na akawaachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni au pesa taslimu Sh15 milioni. Pia aliamrishwa asikanyage afisi za shirikisho au kuzungumza chochote kuhusu kesi hiyo.

Nick Mwendwa akiwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi kuhusiana na ubadhirifu wa fedha za FKF. PICHA | MAKTABA

Baada ya kuondoka kortini Mwendwa alijiuzulu kutoka kwa wadhifa wa Rais FKF na kumpa Naibu wake Doris Petra kuongoza FKF.

Muda huu wote, Fifa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ziliandika barua zikikashifu hatua ya serikali ila hakuna marufuku Kenya iliangushiwa jinsi maafisa wa FKF walivyokuwa wametabiri.

Baada ya kuondoka kwa Mwendwa na sarakasi zilizoandamana na utawala wake, mechi za ligi zilirejelewa, Ligi Kuu na NSL zikirejelewa Disemba 4 huku WPL ikianza Disemba 18.

Kutimuliwa kwa Mwendwa kulifurahisha AFC Leopards na Gor Mahia ambazo mnamo Julai 31 zilisusia Debi ya Mashemeji zikilalamikia kutolipwa Sh1 milioni na Sh2 milioni mtawalia za Kombe la Betway Cup.

Kutokana na kukosa mechi hiyo Mwendwa alitoza Gor faini ya Sh4 milioni huku Leopards ikiadhibiwa kwa faini ya Sh6 milioni na pesa hizo zilikatwa kutoka kwa ufadhili waliokuwa wakiupokea kila mwezi kutoka mdhamini wa ligi BetKing. Hata hivyo, timu hizo mbili baadaye zililipwa pesa zao.

Kuondoka kwa Mwendwa pia kulikuwa mwanzo wa kampuni zilizokuwa zikifadhili ligi kama BetKing, StarTimes na Odibets kubanduka na hadi sasa ligi haina udhamini wowote.

You can share this post!

KWA KIFUPI: Chanjo ya corona inaisha makali baada ya miezi...

Duale awaongoza wabunge wa ‘Tangatanga’...

T L