• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 9:13 AM
Gachagua apotezea Kenya Kwanza kura

Gachagua apotezea Kenya Kwanza kura

NA BENSON MATHEKA

MWANIAJI mwenza wa muungano wa Kenya Kwanza, Bw Rigathi Gachagua, anaonekana kuvuruga muungano huo kwa matamshi yanayokwaza wafuasi na vinara wa vyama tanzu vinavyounga azima ya urais ya Naibu Rais William Ruto.

Ingawa Dkt Ruto amemtetea kwa kusema anaeleweka visivyo, wadadisi wa siasa wanasema kwamba Bw Gachagua asipopima matamshi yake, huenda akashusha motisha ya washirika na wafuasi wa mkubwa wake na kuathiri vibaya umaarufu wake.

“Kuna hisia miongoni mwa washirika na wafuasi wa Kenya Kwanza hasa katika eneo la Mlima Kenya kwamba Bw Gachagua si mwangalifu anapotamka maneno yake, anaropokwa sana bila kubaini huu ni msimu wa kampeni za uchaguzi na kosa dogo linaweza ‘kuchoma picha’,” asema mchanganuzi wa siasa Isaac Gichuki.

Anaendelea kuwa tangu ateuliwe mgombea mwenza wa Dkt Ruto, mbunge huyo wa Mathira amekuwa akizua mihemko kwa matamshi yake japo ukweli ni kwamba alianza kabla ya kuteuliwa.

“Kuna wakati aliponukuliwa akisema kura za jamii ya Wakamba hazina maana kwa kuwa ni chache. Hii ilikuwa kabla ya kuteuliwa mwaniaji mwenza bila kujua kwamba kila kura ni muhimu na kuna viongozi na wafuasi wa jamii hiyo katika Kenya Kwanza ambao alikwaza,” akasema.

Mnamo Mei 18 wakati wa mazishi ya kaka yake, Reraini Gachagua, Bw Gachagua alitoa kauli iliyochukuliwa na wafuasi wa Kenya Kwanza eneo la Mlima Kenya kama ya kuwadunisha ili waonekane kama wasiokuwa na maono isipokuwa kula mlo tu.

“Tuchinje fahali 35 na kupika wali mtamu ili uliwe kwa nyama. Watu wetu hawataki kitu kingine. Hivi ndivyo ilivyokuwa ikifanyika enzi za utawala wa Moi,” alisema Gachagua.

Bw Gichuki anasema kauli hiyo iliwakumbusha wakazi wa Mlima Kenya hali ngumu waliyopitia chini ya utawala miaka 24 wa marehemeu Daniel arap Moi ambapo uchumi wa eneo hilo uliporomoka na vijana wakakosa kazi kabla ya kuokolewa na utawala wa Mwai Kibaki kuanzia 2002.

Wachanganuzi wanasema kwamba tamko kama hilo linaonyesha kuwa Bw Gachagua hawezi kuwakilisha maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Dkt James Kisilu, matamshi ya Bw Gachagua yanatumiwa na wapinzani wa Dkt Ruto kushambulia Kenya Kwanza katika kampeni.

“Tayari baadhi yao wanaambia wakazi wa kaunti za Mlima Kenya kuwa watakachopata kutoka serikali ya Dkt Ruto na Bw Gachagua ni mlo tu,” akasema.

Mbunge huyo pia amekasirisha vinara wa vyama tanzu vya Kenya Kwanza kwa kile wanachosema ni kuwatenga na kuwadharau katika mikutano ya kampeni.

Baadhi ya vyama tanzu vya Kenya Kwanza kutoka Mlima Kenya ni The Service Party chini ya aliyekuwa waziri Mwangi Kiunjuri, Chama Cha Kazi cha mbunge wa Gatundu, Moses Kuria, Tujiebebe Wakenya cha aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, Democratic Party cha Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Farmers Party cha aliyekuwa katibu wa wizara Irungu Nyakera.

Muungano huo pia unaleta pamoja vyama vya ANC chini ya Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha seneta wa Bungoma Moses Wetangula, Maendeleo Chap Chap cha gavana wa Machakos Alfred Mutua na Chama cha Mashinani (CCM) cha aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto.

Bw Gachagua amekanusha kuwa anabagua vyama tanzu vya muungano huo akisema haviwezi kupewa kipaumbele katika mikutano inayodhaminiwa na United Democratic Alliance (UDA) cha Ruto.

“Hautarajii mtu ahudhurie mkutano wa kisiasa unaopangwa na UDA ambako wawaniaji wetu wametumia pesa kuwahakikisha watu wamehudhuria na utarajie ukumbatiwe,” Gachagua alisema akizungumza katika kituo cha redio cha Inooro FM mapema wiki hii.

Hata hivyo, mwaniaji wa chama kinachounga Kenya Kwanza alisema msimamo wa Bw Gachagua unaenda kinyume na lengo na azima ya muungano huo ambao ni kuunganisha Wakenya kumsaidia Dkt Ruto kushinda uchaguzi na kuunda serikali.

“Haileti picha nzuri kwa sababu kabla yake kuteuliwa, hatukuwa na ubaguzi huu. Anaharibu mambo,” akasema.

Matamshi mengine ya Bw Gachagua ambayo yamezua mdahalo ni kuhusu kampuni kubwa nchini kama Safaricom na Kenya Airways yaliyoashiria hazina faida kwa Wakenya.

Kulingana na Bw Gachagua, serikali ya Kenya Kwanza itakuza biashara ndogo ambazo Wakenya wengi wanashiriki badala ya kuwa na mashirika kama hayo.

“Serikali ya Kenya Kwanza itakuza biashara ndogo ambazo ndizo watu wengi hufanya badala ya kuwa na kampuni kubwa kama Safaricom kulipa ushuru, unaweza kutumia uwekezaji wa kampuni kama hiyo na kubuni kampuni ndogo nyingi zitakazolipa ushuru,” akasema akizungumza na kituo kimoja cha runinga.

Wachanganuzi wanasema matamshi yake yanachukuliwa kuonyesha kuwa serikali ya Kenya Kwanza itakuwa tisho kwa mashirika makubwa ya kibiashara nchini.

Kulingana na Bw Gichuki matamshi ya Bw Gachagua yanaweza kunyima Dkt Ruto kura licha ya umaarufu ambao amejenga kwa karibu miaka mitano.

Hata hivyo, Dkt Ruto anasema matamshi ya Bw Gachagua sio tisho kwa kuwa anaendeleza mfumo wa uchumi wa muungano huo wa kukuza uchumi kuanzia mashinani.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo atarajiwa tena Azimio

DINI: Siri ya kufungua milango iliyofungika

T L