• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
DINI: Siri ya kufungua milango iliyofungika

DINI: Siri ya kufungua milango iliyofungika

NA WYCLIFFE OTIENO

UMEWAHI kutafuta kazi, lakini kila uendapo ni kama mlango umefungwa?

Umewahi kuhitaji kitu sana, lakini ni kama kuna ukuta unaokuzuia kukifikia? Umewahi kusahau au kupoteza funguo ya nyumba yako? Wakumbuka ulivyohangaika, licha ya udogo wa kufuli?

Njia halali ya kuingia mahali popote ni kupitia mlangoni. Yeyote anayeingia kupitia dirishani, bila shaka hawezi kusemekana ameingia kihalali.

Katika maisha kuna milango tunayohitaji kupitia ili kupata tunayohitaji.

Lakini milango iliyofungwa hutuzuia kufikia malengo yetu.Milango iliyofungika hutuzuia kutoka kiwango kimoja hadi kingine. Milango iliyofungika huchelewesha hatima yetu, hukatiza matumaini na kutunyima furaha maishani.Kila lango lina funguo. Kama huna funguo, utahangaika sana kuingia. Kuwa na hekima ni kuwa na funguo.

Mhubiri 10:15 inasema, “Kazi yao wapumbavu huwachosha kila mmoja, Maana hajui hata njia ya kuuendea mji.”

Mhubiri 10:10 inasema, “Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi; Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Walakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa.”

Kusudi la Mungu ni sisi kunawiri kila siku. Mtu hafai kusema kuwa jana ilikuwa nzuri kuliko leo.

Methali 4:18 inasema, Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, Ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu.

Hivyo ni jukumu letu kufanya bidii bila kukata tamaa ili kila milango inayohitajika kufunguka maishani mwetu ifunguke.

Yesu Kristo alitoa mfano wa mtu aliyemwendea rafiki yake akiwa na mgeni ili amsaidie na mkate. Lakini alikataa kumfungulia, akimwambia mlango umefungwa na wanalala. Lakini alipoendelea kumwomba ilibidi afungue na kumpa alichotaka ili asiendelee kuwasumbua.

Mathayo 7:7,8 inasema, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.”

Kuna milango inayofunguliwa na wanadamu, lakini pia kuna milango ambayo Mungu pekee ndiye awezaye kufungua. Hivyo ni muhimu kusali bila kukoma. Waombe watu, muombe Mungu. Tafuta kwa watu, tafuta kwa Mungu, Bisha milango ya watu, bisha lango la Mungu. Usipokata tamaa, Mungu atakufungulia huo mlango.

You can share this post!

Gachagua apotezea Kenya Kwanza kura

Real Madrid wazamisha Liverpool na kunyanyua taji la UEFA...

T L