• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Hatima ya Ruto kuamuliwa katika NDC ya Jubilee Novemba 30.

Hatima ya Ruto kuamuliwa katika NDC ya Jubilee Novemba 30.

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Jubilee kitafanya Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wake (NDC) mnamo tarehe 30 mwezi huu katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi.

Kwenye ilani iliyochapishwa magazetini jana, Katibu Mkuu Raphael Tuju alitaja ajanda za kongamano hilo kuwa; mabadiliko ya katiba na kanuni kadha za chama hicho ili ziambatane na Katiba ya Kenya, Sheria ya Vyama vya Kisiasa na Sheria ya Uchaguzi.

“NDC pia itashughulikia masuala mengine ambayo yatawasilishwa kwake na Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) na Kamati ya Kitaifa ya Uongozi (NGC) ,” akasema. Bw Tuju alitangaza kuwa masharti yote ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa Covid-19 yaliyotolewa na Wizara ya Afya yatazingatiwa katika kongamano hilo litatakalo hudhuriwa na zaidi ya wajumbe 3,000.

Kongamano hilo litaongozwa na kiongozi wa Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta.Wiki jana kundi la wabunge wa Jubilee (PG) walitangaza kuwa wajumbe wa chama hicho wataishinisha kuondolewa kwa Naibu Rais William Ruto kama mwanachama na naibu kiongozi wake.

Hii ni kwa sababu Dkt Ruto na wandani wake wameasi chama hicho na kujiunga na chama pinzani cha United Democratic Alliance (UDA) ambayo wamekuwa wakiivumisha. Wabunge hao pia walisema wadhifa wa naibu kiongozi wa chama utagawanywa ili ushikiliwe na zaidi na mtu mmoja, katika mabadiliko ya Katiba ya Jubilee yatakayoidhinishwa katika NDC hiyo.

Kwenye taarifa waliyotoa baada ya kukutana katika mkahawa wa Safari Park Alhamisi, wabunge hao, wengi wao kutoka eneo la Mlima Kenya, waliwataja waasi waliojiunga na UDA kama watu wasiofaa kuwa viongozi.

“Watu kama hao kwa muda mrefu wamepaka tope chama chetu. Kwa bahati nzuri, Wakenya wameshuhudia wakiungana katika kona ndogo ambako wezi, walaghai, matapeli, maharamia na watu wasiofaa katika jamii wameungana kuwa chama cha kisiasa,” wakasema.

Kongamano hilo la wajumbe wa Jubilee pia linatarajiwa kuidhinisha mchakato wa kubuniwa kwa muungano kati ya chama hicho na ODM. Mkutano huo utafanyika siku 10 kabla ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kuandaa mkutano mkubwa katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi kutangaza kama atwania urais 2022 au la.

Duru zasema kuwa mkutano huo utakaofanyika Novemba 9, 2021 utahudhuriwa na Rais Kenyatta pamoja na wageni wengi kutoka nchini na nje.

You can share this post!

Onyonka avuliwa wadhifa wa Ford Kenya kwa kuunga Raila

Kuna hatari ya Raila ‘kujikwaa’ kisiasa kwa kumtetea...

T L