• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Hofu ya Pwani kususia kura za 2022 yatanda

Hofu ya Pwani kususia kura za 2022 yatanda

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI katika ukanda wa Pwani wameeleza wasiwasi wao kuwa huenda idadi kubwa ya wananchi wakakosa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa sababu ya hasira kuhusu ahadi ambazo hawakutimiziwa.

Katika maeneo tofauti ya Pwani, matatizo kama vile ukosefu wa ajira, uhaba wa maji safi ya matumizi nyumbani, ukame, usalama duni na shida ya kumiliki ardhi kihalali yamekuwa yakijirudia kila mwaka licha ya viongozi wa maeneo hayo na kitaifa kuahidi kuyatatua.

Akizungumza wakati wa kuzindua shughuli ya kuhamasisha umma kujisajili kuwa wapigakura, Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, alisema kususia kura hakutasaidia kutatua matatizo yaliyopo.

Alikuwa ameandamana na wanasiasa mbalimbali wa Mombasa wakiwemo madiwani.

“Tunapoanza safari hii, wakumbusheni wananchi kwamba baadhi ya suluhu hazitapatikana kama wanafanya maamuzi kwa hasira. Tusisusie kura kwani ni jukumu letu kama wananchi kushiriki ili kuhakikisha sauti zetu zimesikika. Sasa tujitokeze tuhimize watu wajitokeze kujisajili kuwa wapigakura,” akasema Bw Joho.

Kaunti ya Mombasa ni miongoni mwa maeneo ambayo kufikia sasa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imepokea idadi ndogo ya wananchi wanaotaka kujisajili upya kuwa wapigakura.

Kulingana na takwimu za IEBC, tume hiyo inalenga kusajili wapigakura wapya 234,741 Mombasa, 199,428 Kwale, na 331,889 Kilifi.

Katika Kaunti ya Tana River, tume hiyo inalenga wapigakura wapya 44,771, huku ikilenga watu 18,179 Lamu, na 69,063 Taita Taveta.

Usajili huo ulioanza Jumatatu unafanywa katika kila wadi nchini kwa siku 30, ikiwemo wikendi.

Katika Kaunti ya Kilifi, maafisa wa IEBC walieleza hofu kuwa ukame ambao unashuhudiwa katika maeneo ya kaunti hiyo huenda ukaathiri usajili.

“Kutokana na jinsi hali ilivyo katika eneobunge la Ganze, Kaloleni na Magarini, huenda wakazi wakakosa kujitokeza kujiandikisha kwa sababu mtu hawezi kuja hapa kusubiri kusajiliwa ilhali hajui jioni atakula nini,” alisema afisa mshirikishi wa uchaguzi katika Kaunti ya Kilifi, Bw Abdulwahid Hussein.

Zaidi ya wadi 16 za Kaunti ya Kilifi zimeathirika na ukame uliosababishwa na kiangazi cha muda mrefu.

Afisa huyo alisema kufikia Alhamisi, watu 2,919 walikuwa wamejisajili ilhali lengo ni kusajili takriban watu 3,900 kila siku.

Bw Hassan Kibwana ambaye ni afisa wa mipango katika shirika la kijamii la Kenya Community Support Centre (KECOSCE) aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kusajiliwa ndipo watimize haki yao ya kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Ninajua kuna changamoto nyingi zinazowakumba wakazi kwa sasa ikiwemo uhaba wa chakula ila ninawaomba jitahidini kujikwamua ili muweze kujitokeza kwa wingi kujisajili. Ni kupitia njia hii ndipo tutaweza kubadilisha hali hii inayowakumba kwa sasa,” alisema Bw Kibwana.

Idadi kubwa ya wananchi wanaolengwa kujisajili ni vijana ambao hawakuwa wametimiza umri wa kushiriki uchaguzi uliopita mwaka wa 2017.

Katika Kaunti ya Lamu, wakazi wa vijiji vya msitu wa Boni ambao umekumbwa na changamoto tele za kiusalama bado hawajaanza kujisajili.

Katika mahojiano, Meneja wa IEBC Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Adan, alisema vifaaa vya kusajili wapigakura wapya havijafika msituni Boni kutokana na hofu za kiusalama.

Bw Adan alisema tayari amezungumza na maafisa wa idara ya usalama ili makarani wa IEBC wapewe ulinzi kuwezesha wakazi kushiriki shughuli hiyo ambayo ni haki yao kidemokrasia.

“Kwa sasa vifaa vya kusajili wapiga kura bado tumevihifadhi katika afisi yetu mjini Faza. Nimezungumza na wahusika wa usalama ili kutusaidia kusafirisha vifaa na makarani wetu msituni Boni ili wakazi wa pale pia waanze shughuli ya kujisajili. Tatizo kuu ni utovu wa usalama ambao umekuwa ukishuhudiwa lakini kila kitu kitakuwa shwari,” akasema Bw Adan.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alisema juhudi zinaendelezwa ili makarani wafikishwe enbeo hilo na wakazi wapate fursa ya kujisajili.

“Tutatumia mbinu zote kuhakikisha wakazi wa msitu wa Boni pia wanashiriki shughuli muhimu kujisajili kupiga kura. Wasiwe na shaka. Tunawashughulikia,” akasema Bw Macharia.

Ukanda wa Pwani ni mojawapo ya maeneo nchini ambayo wagombeaji urais hung’ang’ania kura ikizingatiwa kuwa wakati mwingi hakuna mwenyeji anayewania urais ikilinganishwa na maeneo mengine ya nchi yaliyo na idadi kubwa ya wapigakura.

Ripoti za Wachira Mwangi, Alex Kalama na Kalume Kazungu

You can share this post!

Ufaransa kukutana na Uhispania kwenye fainali ya UEFA...

KIKOLEZO: Blanda za R. Kelly