• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
JAMVI: Gumzo la ugombea-wenza Mlima Kenya lilivyo kiazi moto kwa vigogo

JAMVI: Gumzo la ugombea-wenza Mlima Kenya lilivyo kiazi moto kwa vigogo

Na WANDERI KAMAU

MIUNGANO mikuu ya kisiasa inayoendelea kuchipuka nchini, iko kwenye njiapanda kuhusu wanasiasa itakaowateua kama wagombea-wenza kutoka ukanda wa Mlima Kenya.

Eneo hilo linapigiwa upatu kuchukua nafasi hiyo kwenye kila muungano unaojaribu kubuni ushirikiano wa kisiasa nalo.

Kufikia sasa, miungano na vigogo wa kisiasa ambao wameonyesha dalili za kuwania urais 2022 ni kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, Naibu Rais William Ruto na muungano unaowashirikisha wanasiasa Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Baringo).

Jumapili iliyopita, mwanasiasa Peter Kenneth alisema kuwa lazima eneo hilo litwae ugombea-wenza kwenye muungano wowote litakaobuni ushirikiano nao, ili “kuhakikisha maslahi ya wenyeji wake yamelindwa.”

Bw Kenneth alisema ikizingatiwa ukanda huo una karibu wapigakura milioni sita, halitakubali kubuni ushirikiano wowote na kiongozi ambaye hataliachia ugombea-wenza.

“Mlima Kenya si eneo hivi hivi tu. Huenda tusiwe na mgombea urais 2022 lakini lazima maslahi yetu yalindwe kwa msingi wa idadi yetu kubwa. Anayetutaka lazima atuhakikishie atakachotupa na kututengea ndipo tumuunge mkono,” akasema Bw Kenneth.

Kauli yake imezua hisia mbalimbali miongoni mwa viongozi na wenyeji, wengi wakimuunga mkono kuwa huenda mwelekeo wa kisiasa katika ukanda huo ukaamuliwa na muungano utakaoupa nafasi kubwa kwenye uchaguzi huo.

Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee (JP), Bw David Murathe, anasema kuwa hawatakubali “mtu yeyote kuwavamia vivi hivi tu” kwani lazima awahakikishie wenyeji maslahi yao katika serikali ijayo.

“Ukanda huu ni kama msichana anayechumbiwa na watu wengi. Msimamo wake kuhusu mchumba litakaomchukua ni kulingana na kiwango cha posa atakachoweka,” akasema Bw Murathe, kwenye mahojiano na ‘Jamvi la Siasa.’

Mwelekeo huo umeonekana kuanza kuwapa tumbojoto vigogo wakuu ambao wametangaza azma zao, wengi wakielezwa kuanza mikakati mpya ya kisiasa kujaribu kuwarai wenyeji kuwaunga mkono.

Hadi sasa, Dkt Ruto ndiye amekuwa akionekana kupata uungwaji mkono mkubwa ikilinganishwa na vigogo wengine, kutokana na ziara nyingi za kisiasa ambazo amekuwa akifanya katika eneo hilo.Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa, juhudi zake zimekuwa zikipigwa jeki na wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao wamekuwa wakimsaidia kujipigia debe.

Wiki mbili zilizopita, Gideon pia alionekana kuanza kupenyeza ndoano zake katika eneo hilo, baada ya kuongoza hafla ya kutawazwa kwa Askofu Paul Njenga katika Kanisa la AIPCK Githunguri, Kaunti ya Kiambu.

Kabla ya hapo, Gideon alikuwa amekutana na vijana kutoka kaunti iyo hiyo katika eneo la Ruaka.Kwenye hafla hizo mbili, aliwarai wenyeji kuunga mkono ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).Hata hivyo, duru zilieleza ziara zake zilikuwa na “baraka” kutoka Ikulu ya Nairobi.

Kando na Gideon, mabwana Musyoka na Mudavadi pia wamekuwa wakizuru katika sehemu mbalimbali katika ukanda huo, wakiwaahidi wenyeji “kuwapa nafasi kubwa ya uwakilishi” ikiwa watawaunga mkono kwenye azma zao kuwania urais 2022.

Licha ya ahadi hizo, wadadisi siasa wanasema kuwa licha ya migawanyiko inayoendelea kujitokeza miongoni mwa wanasiasa tofauti eneo hilo, kuna uwezekano wenyeji wakamuunga mkono kiongozi atakayewahakikishia mgao mkubwa wa serikali yake.

Baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakipendekezwa kuwa wagombea-wenza wa miungano hiyo ni Bw Kennth, aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Mwangi wa Iria (Murang’a), aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo kati ya wengine.

Bw Kiunjuri amekuwa akihusishwa na Dkt Ruto huku Bw Kenneth akihusishwa na Bw Odinga.Wadadisi wanasema kuwa kutawazwa kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kama msemaji wa ukanda huo kunatarajiwa kuibua mwelekeo mpya wa kisiasa.

“Ilivyo sasa, Mlima Kenya inapigania ugombea-wenza kwani ni dhahiri kuna uwezekano mkubwa isiwe na mgombea urais baada ya Rais Kenyatta kung’atuka mnamo 2022. Inavyoelekea, ahadi na hakikisho itakazopewa na miungano itakayojitokeza ndizo zitaamua muungano ambao wenyeji watakouunga mkono,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kulingana naye, ukanda huo ni miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya wapigakura nchini, hivyo wenyeji pia wana jukumu la kuwachagua viongozi watakaowatetea vizuri kuhakikisha maslahi yao yamelindwa.

“Ni lazima wenyeji vile vile wafahamu kuwa maslahi yao yatashughulikiwa kwa msingi wa kiongozi watakayemwidhinisha kuwa msemaji wao. Hivyo, lazima miungano pia iwashirikishe wananchi ili kutomteua kiongozi ambaye atakubalika virahisi,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye pia ni mdadisi wa siasa.

Mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ inaonekana kuwa na ushindani mkubwa kuhusu kigogo atakayelinda maslahi ya ukanda huo.Tangatanga wanashikilia Dkt Ruto ndiye anayefaa zaidi, huku ‘Kieleweke’ wakisema Rais Kenyatta ndiye atakayetoa mwelekeo kwa wenyeji kuhusu muungano utakaowafaa zaidi.

You can share this post!

JAMVI: Changamoto tele kwa Kenyatta akijaribu kuzima ndoto...

JAMVI: Raila anawazia nini iwapo atasalitiwa na Rais...