• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
JAMVI:  Ruto mbioni kudhibiti hali Bondeni

JAMVI: Ruto mbioni kudhibiti hali Bondeni

Na WANDERI KAMAU

“Mambo yalivyo sasa, Dkt Ruto hana lingine ila kuhakikisha kuwa ana uungwaji mkono wa kutosha katika jamii hizo, kabla ya kupanua mabawa yake kisiasa katika maneo mengine nchini,” asema Bw Kiprotich Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za Bonde la Ufa.

NAIBU Rais William Ruto ameanza mikakati ya mapema kuunganisha jamii za kuhamahama, maarufu kama KAMATUSA ili kuimarisha mpango wake kuwania urais mnamo 2022.

Mikakati hiyo pia inalenga kudhibiti uungwaji mkono wake kisiasa miongoni mwa jamii hizo kutokana na mawimbi ya kisiasa yanayomkabili katika Chama cha Jubilee (JP) na suitafahamu iliyopo kuhusu hatima yake kufuatia kuzinduliwa kwa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

Muungano huo unazishirikisha jamii za Wakalenjin, Wamaasai, Waturkana na Wasamburu.

Mnamo Ijumaa, zaidi ya viongozi 100 walikutana mjini Naivasha, ambapo walitoa kauli ya pamoja kumuunga mkono licha ya changamoto zinazomkumba.

Miongoni mwa viongozi wakuu waliofika ni Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen, magavana Stephen Sang (Nandi), Jackson Mandago (Uasin Gishu), Paul Chepkwony (Kericho) kati ya wengine.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wote wa kisiasa katika Bonde la Ufa wanaoegemea upande wa Dkt Ruto, viongozi wa kidini, wanataaluma na viongozi wa kijamii wenye ushawishi katika eneo hilo.

Na ingawa viongozi hao hawakueleza moja kwa moja ajenda zao, wadadisi wanasema kuwa Dkt Ruto “anarejea nyumbani kulainisha hali.”

“Mambo yalivyo sasa, Dkt Ruto hana lingine ila kuhakikisha kuwa ana uungwaji mkono wa kutosha katika jamii hizo, kabla ya kupanua mabawa yake kisiasa katika maneo mengine nchini,” asema Bw Kiprotich Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za Bonde la Ufa.

Kikao hicho kinajiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuandaa mkutano wa faragha na viongozi wa kisiasa wa Mlima Kenya katika hoteli ya Sagana Lodge katika Kaunti ya Nyeri mwezi uliopita, ambapo aliwarai viongozi hao kuunga mkono juhudu zake katika kuiunganisha nchi. Kulingana na wadadisi, kikao hicho pia kimesukumwa na madai kwamba Rais Kenyatta anamwandaa kisiri Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kuwania urais mnamo 2022.

Rais Kenyatta amekwepa kuzungumzia kuhusu atakayemrithi baada yake kung’atuka uongozini, licha ya kutoa hakikisho kuwa atamwachia Dkt Ruto usukani baada ya kumaliza kipindi chake.

Wandani wa Dkt Ruto pia wamekuwa wakiwalaumu baadhi ya mawaziri kwa “maonevu ya wazi” dhidi yao.

Mawaziri hao ni Dkt Matiang’i, Joe Mucheru (Habari, Mawasiliano na Teknolojia) na James Macharia (Uchukuzi).

Kulingana na Seneta Samson Cherargei wa Nandi, mawaziri hao wamekuwa wakimkaidi Dkt Ruto kiwazi, licha ya kuwazidi kimamlaka kulingana na katiba.

“Tutaangazia kwa kina mwelekeo tutakaochukua dhidi ya mawaziri hao kwani lengo lao ni kutimiza malengo ya kisiasa ya baadhi ya maafisa wakuu serikalini kwa kutuhangaisha bila sababu zozote,” akasema Bw Cherargei.

Majuzi, seneta huyo alifikishwa mahakamani kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi, jambo alilomlaumu Dkt Matiang’i kuwa mhusika mkuu.

Alidai kuwa waziri huyo amekuwa akitumia mamlaka yake kuwalenga wanasiasa wanaomuunga mkono Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema kuwa mkutano wa Dkt Ruto unajiri katika wakati ufaao, kwani ni dhahiri kwamba Rais Kenyatta anaendelea kumtenga kuhusu masuala makuu yanayohusu serikali.

Viongozi hao wanataja hatua ya kutengwa kwa Dkt Ruto kwenye shughuli za uzinduzi wa ripoti hiyo katika Jumba la Bomas kama ishara tosha kuwa ametengwa kabisa na lazima aanze harakati za kujipanga upya kisiasa.

“Ilivyo sasa, ni dhahiri kuwa lazima Dkt Ruto aanze kutathmini mwelekeo mpya kisiasa kwani mustakabali wake ni mfinyu sana katika Chama cha Jubilee (JP). Kimsingi, ni sahihi kusema kwamba chama hicho hakipo tena,” asema Bw Kipkorir Menjo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za eneo la Bonde la Ufa.

Bw Menjo anasema kuwa “vita baridi” dhidi ya Dkt Ruto vilianza wakati wakurugenzi wakuu wa mashirika mbalimbali ya serikali kama Dkt Ben Chumo wa Kampuni ya Umeme (KP), Dkt Ken Tarus wa Kampuni ya Kuzalisha Kawi (KenGen) kati ya wengine walianza kutolewa katika nyadhifa zao kwa tuhuma za ufisadi katika hali tatanishi.

Asema kwamba, ingawa ilikuwa mapema kutabiri kuwa hali ingefikia ilivyo, kuna uwezekano Rais Kenyatta alifahamu kuhusu njama iliyokuwepo.

Na licha ya hali ngumu ya kisiasa anayokabiliwa nayo kwa sasa, wadadisi wanasema kuwa huenda Dkt Ruto akaigeuza kujiimarisha kisiasa kama alivyofanya Rais Mstaafu Daniel Moi alipokabiliwa na wanasiasa kutoka Mlima Kenya kati ya 1976 na 1978 kupitia wimbi la ‘Change the Constitution Movement’ (Juhudi za Mageuzi ya Katiba).

“Bw Moi alivumilia mateso aliyofanyiwa na wanasiasa kama Kihika Kimani, Njenga Karume, Dkt Munyua Waiyaki kati ya wengine waliolenga kuhakikisha kuwa wanageuza katiba ili kumzuia Bw Moi kumrithi Mzee Kenyatta. Hata hivyo, Moi aliwashinda kutokana na uvumilivu wake,” asema Bw Menjo.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wanaompinga waliandaa kikao sambamba katika eneo la Rongai, Kaunti ya Kajiado, wakishikilia kuwa si Dkt Ruto atakayetoa mwelekeo wa kisiasa kwa jamii hizo.

Kikao hicho kiliwashirikisha wabunge William Kamket (Tiaty), Alfred Keter (Nandi Hills), Joshua Kutuny (Cherangany) kati ya wengine.

You can share this post!

JAMVI: Safari ya BBI kutoka Bomas hadi Bungeni

Polisi walimvunjia Sonko heshima Voi – Raila

adminleo