• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Joto la atakayevalia viatu vya Raila lashamiri

Joto la atakayevalia viatu vya Raila lashamiri

NA CHARLES WASONGA

SENETA wa Siaya Oburu Oginga sasa amekana madai ya kumpendekeza Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi kuwa mrithi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga kama kinara wa kisiasa wa jamii ya Waluo.

Kwenye taarifa Dkt Oginga, ambaye ni kaka mkubwa wa Raila, amefafanua kuwa hajawahi kumtawaza mwanasiasa yeyote kutwaa wadhifa huo, kiongozi huyo wa ODM atakapostaafu siasa.

“Hamna pengo la uongozi wa kisiasa katika jamii ya Waluo la kujazwa wakati huu. Raila bado anashikilia usukani na anafanya vizuri,” seneta huyo akasema.

Dkt Oginga alisema kauli aliyoitoa wiki jana ilifasiriwa visivyo na vyomba vya habari.

Seneta huyo wa Siaya alinukuliwa akisema hivi: “Viongozi hukua kama uyoga. Huchipuza kama uyoga na hivyo ndivyo Opiyo anavyokua na hakuna kitakachomzuia kupata uongozi wa juu kwa sababu sasa tumemwachia. Hawa ndio watu ambao sasa watatuongoza na kutupa mwelekeo.”

Dkt Oginga alisema alipohutubia hafla moja katika eneo bunge la Ugunja mnamo Agosti 23, 2023.

Dkt Oginga akaendelea: “Tumemwona aking’aa na kile tunachopaswa kufahamu ni kwamba viongozi hawachaguliwi, Waluo waliketi wapi na kumchagua Raila kama kiongozi wao?”

Isitoshe, seneta huyo alimtaja Wandayi kama mwanasiasa mwerevu na ambaye amejifunza siasa kutoka kwa Raila.

Kauli ya Dkt Oginga hiyo ilionekana kama iliyotoboa iliyokuwa fiche kuhusu urithi wa Raila na uwezekano wake wa kustaafu kutoka siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Hii ndio maana siku chache baada ya Oginga kutoa kauli hiyo, uongozi wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo ulifanya mkutano mnamo Agosti 25 ambapo duru zasema suala hilo lilijadiliwa kwa kina.

Mkutano huo ulifanyika katika mkahawa wa Pinecone katika mtaa wa Tom Mboya na kuhudhuriwa na mwenyekiti wa baraza hilo Ker Odungi Randa, naibu wake James Ayaga na wengine. Vile vile, alikuwepo mwenyekiti wa muungano wa wabunge kutoka Jamii ya Waluo Mbunge wa Seme Dkt James Nyikal.

Lakini kwenye taarifa yake Jumatatu, Dkt Oginga alisema inasikitisha kuwa kauli yake ya Agosti 23 ilifasiriwa kuwa amemwidhinisha Wandayi kuwa mrithi wa Raila mwenye umri wa 78 sasa.

Akaeleza: “Kile nilichofanya ni kumhimiza tu Bw Wandayi atie bidii. Sikumtawaza. Nilisema anaendelea vizuri na ni miongoni mwa wandani wa Raila ambao wanapaswa kutizamwa kwa makini siku za usoni.”

Dkt Oginga alisema kuwa suala la urithi halifai kuibua mjadala au wasiwasi wakati huu kwani “litajitokeza siku zijazo.”

“Tuko na viongozi wengi wenye umri mdogo ambao wanaweza kuchipuza alivyofanya Raila. Wote wanayo nafasi sawa ya kuongoza,” akasema huku akisisitiza kuwa Raila hakuchaguliwa na yeyote bali “alijikuza mwenyewe”.

Lakini alifafanua kuwa viongozi wenye umri unaokaribiana na ule wa Raila wana nafasi finyu ya kuwa mrithi wake.

“Mbona mwaongeza kuhusu Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o na Gavana wa Siaya James Orengo, kama watu wanaopigiwa upatu kuwa warithi. Hawawezi kwa sababu umri wao ni mkubwa,” akasema.

 Dkt Oginga aliongeza kuwa baadhi ya wale wanaopendekezwa kama warithi wa Raila kwa sababu “hawajaiva kisiasa”.

Huenda Seneta huyo wa siasa alikuwa akirejelea baadhi ya wanasiasa kimbukeni ambao pia majina yao yanatajwa kuwa miongoni mwa wale wanaopigiwa upatu kumrithi Raila kama kiongozi wa kisiasa wa jamii ya Waluo.

Wao ni Mbunge wa Embakasi Babu Owino, Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, bintiye Raila Winnie Odinga na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.

Wengine ambao huenda wamefeli kulingana na Dkt Oginga, kwa misingi ya kuunga mirengo hasimu wa kisiasa ni; Gavana wa zamani wa Nairobi Evans Kidero, Waziri wa ICT Eliud Owalo na Katibu katika Wizara ya Usalama Raymond Omollo.

Kauli ya Oginga inajiri wakati ambapo siasa za urithi zimeshika kasi katika eneo la Luo Nyanza imegeuka kiazi moto, huku wanasiasa wengi wakichelea kulizungumzia hadharani.

Lakini hatua ya seneta huyo kummiminia sifa Wandayi haikuwafurahisha baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Luo Nyanza waliodai anampendelea kiongozi huyo wa wachache bunge.

Wanaonya kuwa hali hiyo inaweza kuleta migawanyiko na mivutano ya kisiasa katika eneo hilo ambalo limedumisha umoja kisiasa kwa muda mrefu nyuma ya Raila.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) alidai kuwa kauli ya Oginga ilitolewa kwa nia mbaya.

Mbunge huyo maalum alipuuzilia mbali kauli ya Seneta huyo wa Siaya kwamba Wandayi anatosha kumrithi Raila akimtaja mbunge huyo wa Ugunja kama “limbukeni kisiasa miongoni mwa wanasiasa kutoka jamii ya Waluo wakati huu.”

“Wandayi bado ni mchanga katika siasa kuweza kuunganisha viongozi wote kutoka Luo Nyanza, jinsi Raila amefanya kwa miaka mingi. Madai kuwa naweza kuwa mrithi ni ndoto tu ambazo haziwezi kutimia,” Bw Mbadi ambaye ni mbunge wa zamani wa Suba Kusini akasema.

Lakini kwenye mahojiano na Taifa Leo, Wandayi amemshukuru Dkt Oginga kwa kutambua uwezo wake kisiasa na kiuongozi.

“Napokea pendekezo la Dkt Oburu kwa moyo mkunjufu na ninamshukuru kwa hilo. Nitajizatiti kupokea wito huo wa kunitaka nitwae uongozi wa eneo la Luo Nyanza kisiasa,” Mbunge huyo akasema.

Bw Wandayi anahudumu muhula wake wa tatu kama Mbunge wa Ugunja. Katika bunge la 12 alihudumu kama mwenyekiti wa kamati ya PAC kwa kipindi cha miaka mitano.

Mwaka 2022, alionyesha nia ya kuwania ugavana wa Siaya, lakini duru zilisema kuwa Raila alimshauri ajiondoe ili kumpisha Bw Orengo.

Wakati huu, Bw Wandayi, 52, anashikiliwa wadhifa wa Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa katika chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

  • Tags

You can share this post!

Wadukuzi wageuza Kenya mlo wao CA ikijitahidi kuziba mianya

Mashamba ya wakazi yazamishwa na uvunaji mchanga Mto Nzoia

T L