• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Juhudi za Raila kuokoa chama cha Jubilee

Juhudi za Raila kuokoa chama cha Jubilee

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, jana aliongoza viongozi wengine wa muungano huo kuokoa afisi za chama cha Jubilee zilizotwaliwa na mrengo uliofanya mapinduzi majuzi.

Akiandamana na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa Narc Kenya na Eugene Wamalwa wa DAP –Kenya miongoni mwa wengine, Bw Odinga alimsindikiza Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni katika makao makuu ya chama hicho aliyepata agizo la mahakama kusitisha kutimuliwa kwake ofisini.

Katika agizo hilo, Jopo la Kuamua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa lilizima hatua ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Anne Nderitu kuidhinisha kutimuliwa kwa Bw Kioni, Naibu Mwenyekiti David Murathe na maafisa wengine wanaounga Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Bi Nderitu alikuwa ametambua mrengo unaoongozwa na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Kanini Kega na mbunge wa kuteuliwa Sabina Chege uliofanya mkutano katika kaunti ya Nakuru na kutimua Bw Kioni na kundi lake.

Hatua ya Bw Kega na wenzake ilijiri baada ya kukutana na Rais William Ruto katika ikulu ya Nairobi na kutangaza kwamba wangeunga serikali.

Jana Alhamisi, Bw Odinga alisisitiza kuwa masaibu ya Jubilee yanatokana na mipango ya Rais Ruto ya kuua demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa nchini na akaonya Wakenya kuwa wataumia iwapo atafaulu.

“Kuna vitisho kwa demokrasia ya vyama vingi nchini kwa kulemaza na kusambaratisha vyama vya kisiasa. Utawala wa sheria na Katiba uko katika hatari kubwa,” alisema Bw Odinga.

Bw Kioni alisema kwamba majaribio ya kutwaa chama cha Jubilee yalianza Juni 2022 kupitia juhudi za kusajili Jubilee Asili.

“Kumekuwa na majaribio kadha ya kuteka, kuvunja na kuharibu Jubilee tangu mwaka 2022. Zilianza na baadhi ya watu kujaribu kusajili Jubilee Asili lakini wakagonga mwamba,” alisema.

Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragwa alisema juhudi hizo zilifufuliwa katika mkutano wa Rais Ruto na wabunge waasi wa chama hicho katika ikulu akidai ndio ulipanga njama ya mapinduzi yaliyofanywa na kundi la Bw Kega mjini Nakuru wiki jana,

Alishambulia msajili wa vyama vya kisiasa kwa kuidhinisha mapinduzi hayo akisisitiza ni Katibu Mkuu na Kiongozi wa chama walipatiwa mamlaka na katiba ya Jubilee kuitisha Mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC).

Akilaumu Rais Ruto kwa kupanga kuharibu Jubilee, Bw Kioni alidai kwamba kundi la Bw Kega lilipatiwa ulinzi wa maafisa wa polisi kutwaa afisi za chama hicho mtaani Lavington, Nairobi baada ya kuidhinishwa ‘kiharamu’ na msajili wa vyama vya kisiasa.

“Kwa vile sisi ni wapenda amani na hatutaki hata tone moja la damu limwagike katika mchakato tulioanzisha, tuliagiza waliokuwa katika ofisi kutozua vurugu na leo tumepata agizo la Mahakama na ndio sababu tuko hapa,” akasema.

Alisisitiza kuwa Jubilee ingali imara katika Azimio na inaunga msururu wa mikutano iliyoanza maeneo tofauti nchini.

  • Tags

You can share this post!

Ruto apata fursa ya kutwika raia mzigo

Ichung’wa ahusisha Azimio na wadukuzi wa Israeli

T L