• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Ichung’wa ahusisha Azimio na wadukuzi wa Israeli

Ichung’wa ahusisha Azimio na wadukuzi wa Israeli

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa amewataja viongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya kama wanafiki kwa kudai kuwa walipokonywa ushindi.

Hii ni kufuatia ufichuzi kuwa wadukuzi kutoka Israeli walijaribu kuvuruga akaunti za mitandao za wandani wa Rais William Ruto katika njama ya kufanikisha ushindi wa aliyekuwa mgombeaji urais wa Azimio Raila Odinga.

“Sio jambo la kutushtua kwamba wale ambao wamekuwa wakilalamikia kuibiwa kura katika uchaguzi mkuu ndio watu halisi waliopanga njama ya wizi wa kura kwa usaidizi wa wadukuzi wa mitandao,” Bw Ichung’wa akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi, Februari 16, 2023.

Bw Ichung’wa ambaye ni mbunge wa Kikuyu alimtaka Bw Odinga kukubali kuwa Rais William Ruto ndiye alishinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

“Raila akome kuyumbisha serikali ya Rais Ruto ambaye ushindi wake ulihalilishwa na Mahakama ya Juu. Sasa imebainika ni Raila na wenzake ndio walijaribu kuhujumu ushindi wetu kwa usaidizi wa wadukuzi mitandao kutoka Israel,” akaongeza.

Gazeti la the The Guardian ambalo huchapishwa Uingereza liliripoti Jumatano kuhusu majaribio ya udukuzi yaliyolenga akaunti za mitandao ya kijamii ya wahusika wakuu katika kampeni za Dkt Ruto.

Kulingana na chapisho hilo, majaribio hayo yalianza kufanyika Julai 2022 ambapo wadukuzi hao walilenga anwani za Telegram na Gmail.

The Guardian inadai kuwa Waisraeli hao waliweza kuingilia anwani za baruapepe na mawasiliano ya kibinafsi ya mtaalamu wa kidijitali Dennis Itumbi na Waziri wa Kawi Davis Chirchir, wakati huo akihudumu kama Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi ya Naibu Rais.

Kulingana gazeti hilo, wadukuzi hao waliongozwa na Tal Hanan, raia wa Israeli na afisa wa zamani wa kijeshi nchini humo.

Hanan aliyejulikana kwa jina la msimbo, “Jorge” aliendesha operesheni za udukuzi kutoka eneo moja la kiviwanda lililoko maili 20 kaskazini mwa jiji kuu nchini Israeli, Tel Aviv.

Wakati wa kesi ya kupinga ushindi wa Rais Ruto katika Mahakama ya Juu, Bw Odinga alidai kuwa mitambo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilichakachuliwa kuvuruga matokeo ya urais.

Alidai wahusika walikuwa raia wa Venezuela ambao walikuwa wakihudumia kampuni ya Smartmatic iliyokodiwa na IEBC kusimamia mitambo yake ya kiteknolojia.

  • Tags

You can share this post!

Juhudi za Raila kuokoa chama cha Jubilee

Afueni ya muda kwa Kioni na wenzake waliotimuliwa na kundi...

T L