• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Junet apuuza madai ya mvutano katika kamati ya kuteua naibu

Junet apuuza madai ya mvutano katika kamati ya kuteua naibu

NA CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Junet Mohamed amepuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa mgawanyiko katika kamati ya kuteua mgombea mwenza wa Raila Odinga.

Bw Mohamed alishikilia Jumapili kwamba kamati hiyo inayoongozwa na waziri wa zamani Noah Wekesa iko tayari kuwahoji watu 11 wanaotaka wateuliwe katika nafasi hiyo.

“Ninavyofahamu ni kwamba hali ni shwari katika kamati hiyo na inajitayarisha kuwahoji watu 11 waliotuma maombi. Kufikia sasa sijapata habari kwamba kuna mmoja wa wanakamati hao anayepania kujiondoa,” akasema.

Wasiwasi kuhusu mgawanyiko katika kamati hiyo ya watu saba ulichipuza Jumamosi baada ya Seneta wa Kitui, Enoch Wambua kutisha kujiondoa.

Bw Wambua, ambaye anawakilisha kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, alisema kuwa ni heri ajiuzulu kutoka kamati hiyo ikiwa itabainika kuwa inatumika kuhalalisha uteuzi wa mtu fulani.

“Ikiwa nitachunguza na kugundua kuwa tumewekwa pale tu kuidhinisha uamuzi ambao ulikuwa umefikiwa awali, na ambao sio mzuri, mimi knitajiondoa kutoka kamati hiyo,” akasema akiendesha kampeni katika Kaunti ya Kitui.

“Siwezi kuongea kwa niaba ya kamati hiyo au kwa niaba ya Bw Wambua au mwanachama yeyote. Kile ambacho nafahamu ni kwamba kamati hiyo itafanya mikutano Jumatatu na Jumanne kwa ajili ya kuteua mgombeaji mwenza wa Bw Odinga,” akasema.

Duru zinasema kuwa Seneta Wambua amekerwa na kujumuishwa kwa jina la Gavana wa Kitui, Charity Ngilu katika orodha ya watu watakaoshindania nafasi hiyo.

Wale ambao majina yao yalikuwa yameorodheshwa mbeleni ni Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu), Peter Kenneth (Jubilee), Sabina Chege (Jubilee), Martha Karua (Narc Kenya), Ali Hassan Joho (ODM) na Stephen Tarus (National Liberty Party-NLP).

Wengine ni magavana Lee Kinyanjui (Ubuntu Peoples’ Forum), Wycliff Oparanya (ODM) na Peter Munya (PNU).

  • Tags

You can share this post!

Wafadhili walia Kenya imewapora

MWALIMU WA WIKI: Michael Kipkirui Ng’etich

T L