• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Kalonzo atatiza kampeni za Sonko kwa kuhepa Raila

Kalonzo atatiza kampeni za Sonko kwa kuhepa Raila

NA FARHIYA HUSSEIN

HATUA ya kinara wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kutangaza kuwa atawania urais na kujiondoa katika muungano wa Azimio la Umoja, imewaacha wagombeaji wa viti kupitia chama hicho kwenye mataa.

Mmoja wa wagombeaji ambao watalazimika kupanga upya mikakati yao ya kampeni ni aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, ambaye tayari alikuwa ashamwaga mamilioni ya pesa kwa maandalizi ya kumpigia debe kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kwa urais chini ya muungano wa Azimio la Umoja.

Punde tu alipotangaza azma yake ya kuwania ugavana wa Mombasa katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, Bw Sonko aliingia mjini humo kwa mbwembwe tele kujionyesha kuwa mfuasi mwaminifu wa Bw Odinga.

Hayo ni licha ya kuwa ODM ina mgombeaji wake wa ugavana Mombasa, ambaye ni Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir.

Bw Sonko alionekana na magari ya kifahari yaliyokuwa yamechapishwa nembo za Azimio pamoja na sura ya Bw Odinga, mbali na Bw Musyoka aliyetarajia kuwa mgombea mwenza wake, na Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, ambaye ndiye mgombea mwenza wake wa ugavana.

Uwekezaji huo wote huenda ukawa hasara kwake ikiwa Bw Musyoka ataendelea kushikilia msimamo wake mkali wa kutaka kuwania urais.

Imebainika kuwa kuweka vibandiko vya magari madogo hugharimu kati ya Sh20,000 hadi Sh30,000 kulingana na aina ya vibandiko vitakavyotumiwa.

Katika msafara wake pia alikuwa na malori ya barabarani yenye sura yake na zile za Bw Musyoka na Bw Odinga, ambazo inakisiwa ziligharimu maelfu ya pesa.

Bw Sonko ameashiria kuwa sasa atalenga zaidi utoaji wa misaada kupitia kikosi chake cha Sonko Rescue Team.

“Hata vigogo wa Azimio wakiachana, huduma zetu za Sonko Rescue Team zitaendea kusaidia wote nchini ambao watakuwa wamelemewa na gharama za mazishi ya wapendwa wao bila ya kubagua mtu yeyote yule,” akaeleza.

Mbali na hayo, endapo talaka ya Bw Musyoka katika Azimio itadumu, taharuki ambazo zilikuwa tayari zishaanza kushuhudiwa ndani ya muungano huo katika kinyang’anyiro kati ya Bw Sonko na Bw Nassir huenda zikapungua Mombasa.

Wikendi iliyopita, rabsha zilizuka katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Bw Odinga eneo la Mkomani wakati Bw Sonko alipowasili na wafuasi wake.

Mnamo Jumatatu, Bw Sonko aliandikisha taarifa katika makao makuu ya polisi wa eneo la Pwani kuhusu fujo hizo.

Kulikuwa na milio ya risasi hewani kuwatawanya vijana waliokuwa wakizua ghasia ambao walimzuia kuhudhuria mkutano huo.

Bw Sonko, ambaye alikuwa ndani ya gari dogo lisilokuwa na nambari za usajili, alilazimika kuondoka kwa kasi.

Mwanasiasa huyo alibanduliwa mamlakani Nairobi, baada ya Seneti kukubaliana na Bunge la Kaunti ya Nairobi kwamba alikuwa na makosa mbalimbali ikiwemo ubadhirifu wa fedha na ukosefu wa maadili.

Kwa msingi huo, kesi kadhaa zimewasilishwa katika mahakama mbalimbali kutaka Tume ya Uchaguzi (IEBC) isimwidhinishe kuwania wadhifa wa kisiasa.

Awali, IEBC ilikuwa imesema haiwezi kumzuia kuwania ikiwa bado ana nafasi za kukata rufaa dhidi ya kung’olewa mamlakani.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yaagiza mwanamume, 52, arudishiwe mahari baada ya...

ZARAA: Vitafunio vya wimbi vyazua msisimko sokoni

T L