• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Kalonzo kuachwa kwa mataa

Kalonzo kuachwa kwa mataa

NA LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka anakumbwa na hatari ya kutengwa kisiasa iwapo atafeli kujiunga na muungano wa Azimio la Umoja kesho Jumamosi.

Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga wanatarajiwa kesho kuongoza kikao cha wajumbe wa vyama vilivyo ndani ya Azimio la Umoja katika jumba la KICC na kisha mchana kuelekea uwanjani Jacaranda, Nairobi, kwa ajili ya mkutano mkubwa wa kisiasa.

Bw Odinga atatawazwa rasmi uwanjani Jacaranda kuwa mwaniaji wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja unaojumuisha zaidi ya vyama 10.

Chama cha United Democratic Movement (UDM) kinachoongozwa na Gavana wa Mandera Ali Roba ndicho cha hivi karibuni kujiunga na Azimio la Umoja baada ya kutangaza Alhamisi kuunga mkono Bw Odinga.

Bw Musyoka ameshikilia kuwa atajiunga na Azimio la Umoja iwapo Bw Odinga atamwachia kupeperusha bendera ya muungano huo.

Jana Alhamisi, Bw Musyoka alisema kuwa, huenda akaunga mkono Bw Odinga kwa mara nyingine au awanie kivyake.

Alisema kuwa akiamua kuwania atawanyima Bw Odinga au Naibu wa Rais William Ruto ushindi wa moja kwa moja kwa kuwafanya kutopata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Gavana wa Machakos, Alfred Mutua alidai Alhamisi kuwa kinara huyo wa One Kenya Alliance (OKA) analenga kugawanya kura za Ukambani kwa kuwania urais kwa lengo la kumnufaisha Naibu wa Rais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

Mdadisi wa masuala ya kisiasa Dismas Mokua anasema Bw Musyoka akiwania urais ataumiza Bw Odinga kwa kumpokonya kiasi kikubwa cha kura za eneo la Ukambani.

Bw Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa anasema Bw Musyoka anapigania tiketi ya urais ya Azimio la Umoja kama njia mojawapo ya kutaka kuteuliwa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

“Kalonzo anataka kuteuliwa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga. Lakini ukweli ni kwamba, nafasi hiyo itaendea eneo la Mlima Kenya. Ajiunge na Azimio la Umoja baadaye atapewa wadhifa wowote serikalini muungano huo ukishinda,” anasema.

Vinara wengine wa OKA, Bw Gideon Moi na Bw Cyrus Jirongo (United Democratic Party, UDP) tayari wamesema watahudhuria mkutano wa kesho wa Azimio la Umoja.

Wadadisi wanatabiri kuwa muungano wa OKA huenda ukasambaratika iwapo Bw Musyoka atakosa kutangaza msimamo wake kesho.

Alhamisi, Bw Musyoka alikutana na mwana wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, Jimmy, katika makao ya OKA mtaani Karen, Nairobi, ambapo inaaminika walifanya mazungumzo ya kina kuhusu kumuunga mkono Bw Odinga. Bw Moi pia alihudhuria mkutano huo.

Bw Jimmy Kibaki ambaye ni kiongozi wa chama cha New Democrats Party (NDP) tayari ametangaza kuwa atafuata nyayo za Rais Kenyatta kwa kuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Kulingana na duru ndani ya Azimio la Umoja, Rais Kenyatta na Bw Odinga walimwacha Bw Musyoka kujifanyia uamuzi baada ya kuibuka na masharti mapya wiki iliyopita, ambapo alimtaka kinara wa ODM Raila Odinga kumuunga mkono kwa mujibu wa mkataba wa maelewano waliotia saini kabla ya uchaguzi wa 2017.

“Kalonzo amesalia na mambo matatu: kujiunga na Azimio la Umoja, kuwania urais kivyake na kujiaibisha kwa kupata chini ya asilimia 40 ya kura za Ukambani au kustaafu kutoka kwenye siasa,” anasema Bw Bigambo.

Jana Alhamisi, Bw Moi alisisitiza kuwa angali ndani ya OKA na kutaka mazungumzo ya kujiunga na Azimio la Umoja kufanywa kwa uwazi na uaminifu.

“Kanu hatujatoka OKA. Hatubanduki hadi tuafikiane katika mazungumzo yanayoendelea,” akasema Seneta huyo wa Baringo.

Baadhi ya viongozi wa Azimio la Umoja waliozungumza na Taifa Leo, walidokeza kuwa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamemwachia Bw Moi jukumu la kumshawishi Kalonzo kujiunga na Azimio la Umoja bila masharti.

Kinara huyo wa Wiper amekuwa akishinikizwa na baadhi ya wandani wake kuwania urais kivyake huku kundi jingine likimtaka kujiunga na Azimio la Umoja.

Bw Odinga Jumatatu alisema yeye na Rais Kenyatta hawatalazimisha yeyote kujiunga na muungano wa Azimio la Umoja.

“Huu ni muungano wa watu wenye maono sawa. Watakaohudhuria mkutano wa Jumamosi ni viongozi wanaoamini sera na lengo la Azimio. Hakuna mtu atalazimishwa kujiunga,” alisema Bw Odinga huku akionekana kumlenga Bw Musyoka.

You can share this post!

Ajali kivuko cha Likoni

Kenya Kwanza wataka Timamy awanie ugavana

T L