• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 3:42 PM
Kalonzo tayari ‘kurithi’ Raila kura za 2027

Kalonzo tayari ‘kurithi’ Raila kura za 2027

NA PIUS MAUNDU

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka ametangaza kuwa atawania urais 2027 huku akisema kuwa tayari anaungwa mkono na ngome ya kinara wa Azimio Raila Odinga.

Bw Musyoka amesema kuwa yuko tayari kupambana na Rais William Ruto ili kumzuia ‘kumpokonya’ eneo la Ukambani.

Makamu huyo wa Rais wa zamani, aliwataka wakazi wa eneo la Ukambani kumuunga mkono ili awe na nguvu ya kumshinda Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027.

“Nimeona mengi na jamii ya Wakamba inapasa kusimama imara. Sasa hakuna kitu ambacho kitamzuia Kalonzo kuwa rais wa Kenya. Rais Ruto ndio kizingiti pekee na anafahamu hili. Alisema kuwa anajua kwamba Kalonzo atakabiliana naye katika uchaguzi mkuu wa 2027,” Bw Musyoka akasema katika Shule ya Msingi ya Kisiiki, Kaunti ya Machakos Jumamosi.

Alikuwa amehudhuria hafla ya kusherehekea ushindi wa diwani wa wadi ya Ndalani, Bw Francis Kitaka.

Bw Musyoka alisema amedhihirisha uzalendo kwa kumuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Watu wote kutoka jamii ya Waluo wanasema kuwa ni Kalonzo wanamuunga mkono katika kinyang’anyiro cha urais 2027. Naamini watatimiza ahadi hiyo,” akasema.

Tangazo la Bw Musyoka kuwa atawania urais limejiri miezi mitatu baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 uliowasukuma Mbw Odinga, Musyoka na kiongozi wa Narc Kenya, Bi Martha Karua katika upinzani.

Tangazo hilo pia linajiri huku kukiwa na hali ya kukanganyikiwa miongoni mwa raia katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni ambazo ni ngome za kisiasa za Bw Musyoka.

Isitoshe, kiongozi huyo wa Wiper ametoa tangazo wakati ambapo yeye na wafuasi wake wamekuwa wakishinikizwa kujiunga na muungano tawala wa Kenya Kwanza (KKA).

Japo amepinga shinikizo hizo kutoka kwa Rais Ruto, Bw Musyoka ametetea uamuzi wa magavana Wavinya Ndeti (Machakos) na Mutula Kilonzo Junior, kufanya kazi kwa ukaribu na Rais Ruto.

Anasema magavana hao hawajafanya kosa lolote kufanya kazi na Serikali ya Kitaifa mradi hawajagura Wiper na kujiunga na KKA.

Imearifiwa kuwa kumvutia Bw Musyoka ni mojawapo ya mbinu ambazo Rais Ruto anatekeleza kunyakua ngome hiyo kisiasa.

Kulingana na sajili ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), eneo la Ukambani lina jumla ya kura Sh1.7 milioni.

Kundi la wandani wa Rais Ruto kutoka Ukambani limejitolea kuhimiza wakazi kuunga mkono utawala wa KKA huku likionyesha kutokuwa na imani na Bw Musyoka.

“Jamii ya Wakenya ina nafasi finyu zaidi ya kuingia Ikulu. Tumekuwa kwenye baridi kwa miaka 10. Tunafaa kuunga mkono utawala wa KKA kwa sababu hatuwezi kusalia katika upinzani kwa miaka mingine 10,” Seneta wa zamani wa Kitui, Bw David Musila, alisema juzi.

Bw Musila, ambaye zamani alikuwa mwandani wa Bw Musyoka, ni miongoni mwa viongozi wapya wa Ukambani kujiunga na kambi ya Rais Ruto.

Kambi hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Johnson Muthama.

Kundi hilo linashirikisha wataalamu na wanasiasa, wengi wao wakiwa ni wale waliopoteza katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Wanachama wa kundi hilo wamekuwa wakikutana kupanga mikakati ya kuwezesha watu kutoka eneo hilo kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Wandani hao wa Dkt Ruto pia wanapanga kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya Ukambani kuvumisha ajenda za serikali huku wakiwahimiza wakazi kuunga mkono Rais Ruto.

Wamemtaja Bw Musyoka kama kiongozi anayeendeleza siasa za kufaidi masilahi yake ya kibinafsi na kupotosha jamii ya Wakamba.

  • Tags

You can share this post!

Uhaba wa fedha kukwamisha utoaji pasipoti, Seneti yaelezwa

Usalama waimarishwa Bondeni mitihani iking’oa nanga

T L