• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Kananu aidhinishwa kuwa Naibu Gavana wa Nairobi

Kananu aidhinishwa kuwa Naibu Gavana wa Nairobi

 Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kaunti ya Nairobi hatimaye limeidhinisha uteuzi wa Anne Kananu Mwenda kuwa Naibu Gavana.

Kwenye kikao cha bunge hilo Ijumaa, madiwani waliohudhuria waliidhinishwa ripoti ya Kamati ya Uteuzi ambayo awali, asubuhi, ilimchunguza Bi Mwenda kubaini ufaafu wake kwa wadhifa huo.

Kabla ya uteuzi wake mapema 2020 na gavana wa zamani Mike Sonko, Bi Mwenda amekuwa Afisa Mkuu katika Idara ya Kupambana na Majanga katika serikali ya kaunti ya Nairobi.

Kwa mujinu wa ripoti ya kamati hiyo iliyowasilishwa bunge na kiongozi wa wengi Abdi Guyo, Bi Mwenda aliidhinishwa na asasi hitajika za serikali kama vile Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Bodi ya Kutoa Mikopo kwa Elimu ya Juu (HELB) na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).

“Vile vile, kamati hii imemchunguza Bi Mwenda na kubaini kuwa ametimiza matakwa mengine yote hitajika kwa wadhifa wa Naibu Gavana wa Kaunti ya Nairobi. Kwa hakika ana ufahamu mkubwa zaidi kuhusu utendakazi wa serikali hii,” akasema Bw Guyo alipokuwa akiwasilisha ripoti hiyo.

Sasa Bi Mwenda anasubiri kuteuliwa rasmi na Kaimu Gavana wa Nairobi Benson Mutura na aapishwe kuanza kazi.

Hata hivyo, duru zasema kuwa muda mfupi baada ya kuapishwa kwa wadhifa wa Naibu Gavana Bi Mwenda ataapishwa tena kuwa Gavana wa Nairobi na hivyo kuchukua nafasi ya Mike Sonko.

Sonko alitimuliwa mnamo Desemba 17,2020 baada ya Bunge la Seneti kuidhinisha hoja ya kumtimua iliyopitishwa katika Bunge la Kaunti ya Nairobi mnamo Desemba 3, 2020.

You can share this post!

Mbunge wa zamani kortini kwa wizi wa shamba

Kananu aahidi kuunga mkono BBI