• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 7:55 AM
Karua ahofia kura kurudiwa kama 2017

Karua ahofia kura kurudiwa kama 2017

CECIL ODONGO NA LEONARD ONYANGO

MWANIAJI mwenza wa urais wa muungano wa Azimio Martha Karua sasa anaitaka tume ya uchaguzi kuelezea mikakati iliyoweka kuepuka kubatilishwa kwa matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu ujao.

Bi Karua ambaye ni mwaniaji mwenza wa kinara wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, jana alisema kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inafaa kuwahakikishia Wakenya kuwa makosa ya 2017 yaliyosababisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta kubatilishwa, hayatarudiwa tena.

“Lazima tuelezwe jinsi IEBC inavyopanga kuandaa Uchaguzi Mkuu, vifaa vitakavyotumika na pia namna ambayo imeyashughulikia masuala yaliyosababisha matokeo ya urais ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017 kufutiliwa mbali.”

“Iwapo tume imeyashughulikia masuala hayo, basi lazima tuambiwe kwa sababu imesalia miezi miwili pekee kabla ya kura,” akasema Bi Karua alipokuwa akihutubia mkutano wa mashirika ya kijamii jijini Nairobi.

Mnamo Septemba 1, 2017, Mahakama ya Juu – ambayo wakati huo iliongozwa na Jaji Mkuu David Maraga – ilibatilisha ushindi wa Rais Kenyatta baada ya kubaini dosari tele, ikiwemo kufeli kwa mitambo ya kupeperusha matokeo (Kiems).

Muungano wa NASA ulioongozwa na Bw Odinga, uliususia uchaguzi huo wa marudio uliofanyika Oktoba 26, 2017, ukisema kuwa IEBC haikuwa na uwezo wa kuhakikisha uchaguzi huru na haki.

“Sisi katika Azimio tuna imani kuwa tutashinda uchaguzi huu na tunalenga kutia bidii kuhakikisha kuwa tunawashinda wapinzani wetu kwa kura nyingi kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa 2002,” alisema Bi Karua.

Kwa mujibu wa Katiba, mshindi wa urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 za kura zote zilizopigwa na angalau asilimia 25 katika kaunti 24 nchini.

“Kushinda kwa idadi kubwa ya kura kunaweza kuzuia mambo mengi yanayoibuka kama kesi nyingi na gharama kubwa ya kuwalipa mawakili kusikiliza kesi zinazowasilishwa kortini,” akasema kiongozi huyo wa Narc.

SAJILI

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) chini ya Naibu Rais, Dkt William Ruto tayari kimeandikia barua IEBC kikitaka tume hiyo kuweka wazi sajili ya wapigakura iliyoidhinishwa.

Lakini mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema Ijumaa kuwa kampuni ya KPMG International Limited iliyopewa kandarasi ya kusafisha sajili ya wapigakura, imekamilisha shughuli hiyo.

Sajili hiyo itakabidhiwa rasmi kwa IEBC wiki ijayo kabla ya kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali.Bw Odinga alipokuwa akihutubia wafuasi wake katika uwanja wa Kamkunji, Nairobi, wiki iliyopita, pia alikemea IEBC huku akisema imekuwa ikitoa ‘kadi nyekundu kiholela’ bila kufafanua alichomaanisha.

Jana Ijumaa, Bi Karua alifichua kuwa muungano wa Azimio utaandikia IEBC barua kwa madhumuni ya kupata ufafanuzi kuhusu iwapo tume hiyo imetatua changamoto zilizoshuhudiwa katika uchaguzi uliopita kwa sababu mara hii lazima washindi na walioshindwa waridhike.Katika ripoti yake ya baada ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017, IEBC ilitaja changamoto tele ambazo ziliifanya kufeli.

Ililaumu hatua ya wabunge kubadili sheria za uchaguzi kiholela karibu na uchaguzi, korti kutoa maamuzi yanayohusiana na uchaguzi dakika za mwisho na kesi tele zinazohusiana na zabuni za kununua vifaa vya uchaguzi.

Ili kukwepa baadhi ya changamoto, ilinuia kununua vifaa vya Kiems mwaka mmoja kabla ya uchaguzi ili kutoa nafasi kwa maafisa wa tume hiyo kupewa mafunzo.

Tume hiyo imetoa kandarasi ya ununuzi wa Kiems kwa kampuni ya Smartmatic ya Uholanzi kwa gharama ya Sh4 bilioni.

Vifaa hivyo havijafanyiwa majaribio – hali ambayo imezua wasiwasi kuwa huenda vikafeli na kusababisha kubatilishwa kwa matokeo.

Mswada wa kutaka Kufanyia Mabadiliko Sheria ya Uchaguzi wa 2022, ambao unalenga kuwezesha IEBC kutumia njia mbadala kupeperusha matokeo iwapo vifaa vya Kiems vitafeli, ungali umekwama Bungeni.

Bunge linafaa kwenda likizo ndefu Juni 9, 2022, ishara kwamba huenda usipitishwe.

Lakini Bw Chebukati, anasema kuwa kukwama kwa mswada huo hakutaathiri maandalizi ya uchaguzi.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi wanaume wanavyoporwa mali kwa ahadi za ngono

Antonio Conte kuendelea kuwa kocha wa Tottenham msimu ujao

T L